Kamisheni ya Uchaguzi Somalia yatangaza tarehe mpya ya uchaguzi wa Rais
Kamisheni ya Uchaguzi ya Somalia imetangaza kuwa, uchaguzi wa Rais nchini humo utafanyika tarehe 30 Oktoba mwaka huu.
Akitangaza tarehe hiyo ya uchaguzi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Somalia, Omar Mohamed Abdulle amesema kuwa, uchaguzi huo sasa utafanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Awali uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti.
Mkuu wa Kamisheni ya Uchaguzi ya Somalia amesema kuwa, uchaguzi wa wawakilishi wa Bunge la Somalia na Bunge la Juu la nchi hiyo utafanyika tarehe 24 na 25 za mwezi ujao wa Septemba.
Uchaguzi wa Rais nchini Somalia utafanyika mwezi Oktoba katika hali ambayo, muda wa uongozi wa Rais wa sasa wa nchi hiyo Hassan Sheikh Mohamoud unamalizika tarehe 10 ya mwezi ujao wa Septemba.
Rais Hassan Sheikh Mohamoud ametangaza nia yake ya kutetea kiti chake hicho katika uchaguzi ujao.
Imeelezwa kuwa, muda wa uongozi wa Rais huyo umeongezwa hadi tarehe ya uchaguzi na Kongamano la Kitaifa la Viongozi.
Uchaguzi huo wa Rais unatathminiwa kuwa una umuhimu wa aina yake hasa kwa kuzingatia matatizo yanayoikabili nchi hiyo kwa sasa.
Nchi ya Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika imekuwa ikikabiliwa na machafuko kwa miaka kadhaa sasa huku kundi la wanamgambo wa al-Shabab likitishia pakubwa usalama wa nchi hiyo na hata nchi jirani.
Mbali na ukosefu wa usalama, Somalia imekuwa ikikabiliwa na tatizo kubwa la ukame na baa la njaa hali ambayo imewafanya baadhi ya raia kuikimbia nchi hiyo na kuomba hifadhi ya ukimbizi katika nchi jirani.