Balozi Seif: Hakuna tena mwanya wa mazungumzo Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema kuwa, hakuna sababu za msingi za kurejewa mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa mkwamo wa uchaguzi mkuu wakati tayari tume ya uchaguzi visiwani humo imekwishaitangaza tarehe 20 ya mwezi ujao kuwa ndi siku ya kurejewa uchaguzi huo.
Balozi Seif Iddi amebainisha kuwa, mazungumzo ya pamoja kati ya Rais wa Zanzibar, Dk. Shein na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, kuhusu kufutwa kwa uchaguzi mkuu yalifanyika kwa maombi ya Maalim Seif na kwamba mwishowe yeye binafsi akaamua kujiondoka kwenye maendeleo ya vikao vya mazungumzo hayo. Amesema, kinacholikabili taifa kwa wakati huu ni suala la marejeo ya uchaguzi si njia nyingine na kwamba, walioamua kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio ni vema wakabakia nyumbani ili kutoa fursa kwa wenzao kushiriki kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua viongozi wanaowataka. Hivi karibuni Chama cha Wananchi CUF kilitangaza kuwa, kiko tayari kurudi kwenye mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi wa amani mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar, kwa sharti kwamba, mchakato wa uchaguzi wa marudio usimamishwe. Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia katika mgogoro wa kisiasa mwezi Oktoba mwaka jana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichokiita ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa zoezi la upigaji kura.