Ajali nyingine ya boti yaua watu zaidi ya 60 nchini Nigeria
Kwa akali watu 60 wamefariki dunia baada ya mashua iliyokuwa imebeba zaidi ya abiria 100 kupinduka na kuzama katika jimbo la Niger, kaskazini mwa Nigeria.
Boti hiyo iliondoka Tungan Sule wilayani Malale Jumanne asubuhi, kuelekea mji wa Dugga kwa ziara ya rambirambi, ilipogonga kisiki cha mti kilichokuwa chini ya maji karibu na kijiji cha Gausawa katika eneo la Serikali ya Mtaa la Borgu.
"Idadi ya waliofariki dunia katika tukio la boti imeongezeka hadi 60," Abdullahi Baba Ara, mwenyekiti wa eneo la Serikali ya Mtaa la Borgu aliliambia shirika la habari la Reuters jana Jumatano.
"Watu kumi wamepatikana katika hali mbaya, na wengi bado wanatafutwa." Sa’adu Inuwa Muhammad, Mkuu wa Wilaya ya Shagumi, amesema mara baada ya kufika katika eneo la tukio.
"Boti hiyo ilibeba zaidi ya watu 100. Tuliweza kuopoa maiti 31 majini. Boti hiyo pia imepatikana na kuondolewa majini," amesema afisa huyo na kuongeza kuwa, wanawake na watoto walikuwa miongoni mwa wahanga wa ajakli hiyo.
Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya watu wasiopungua 22 kuaga dunia baada ya boti waliyokuwa wameabiri kuzama katika jimbo la Sokoto, kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Itakumbukwa kuwa, wakulima wasiopungua 16 walikufa maji katika ajali kama hiyo mwezi Agosti 2024 wakati boti yao iliyokuwa inawapeleka kwenye mashamba yao ya mpunga kuzama katika jimbo hilo hilo la Sokoto.