133 wakamatwa na polisi Zambia kwa kupinga ushindi wa Rais Lungu
Polisi nchini Zambia imewatia mbaroni makumi ya wafuasi wa upinzani wanaopinga ushindi wa Rais Edgar Lungu katika uchaguzi wa rais uliofanyika Alkhamisi iliyopita.
Godwin Phiri, mkuu wa polisi katika mkoa wa Kusini ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wafuasi 133 wa chama cha upinzani cha UPND wamekamatwa kwa kupinga matokeo halali ya uchaguzi wa rais, kuwashambulia wafuasi wa chama tawala sambamba na kuharibu mali zao. Aidha amesisitiza kuwa kwa sasa hali ya utulivu imerejea baada ya wafuasi hao wa upinzani kutiwa nguvuni.
Haya yanajiri huku Rais Lungu akifanya mkutano wa hadhara katika eneo la Woodlands karibu na Ikulu ya Rais, mashariki mwa mji mkuu Lusaka, kuwashukuru wananchi kwa kumchagua. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) Jaji Esau Chulu jana alimtangaza Edgar Chagwa Lungu kuwa rais mteule kwa kupata asilimia 50.35 ya kura dhidi ya mpinzani wake Hakainde Hichelema aliyepata asilimia 47.63 ya kura zote.
Hata hivyo kiongozi wa chama cha upinzani cha UPND Hakainde Hichilema amesema kutangazwa mshindi Rais Edgar Lungu ni sawa na mapinduzi ya kijeshi dhidi ya mchakato wa kidemokrasia nchini Zambia.
Hichilema amesisitiza kuwa chama chake kitawasilisha mashtaka katika Mahakama ya Katiba kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zambia akisema matakwa ya wananchi yamechakachuliwa na demokrasia imepuuzwa.