Dak: Machar ametoroka Sudan Kusini kwa kuandamwa na maafisa usalama
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13513-dak_machar_ametoroka_sudan_kusini_kwa_kuandamwa_na_maafisa_usalama
Msemaji wa kiongozi wa upinzani nchini Sudan Kusini amesema Riek Machar ameikimbia nchi hiyo kutokana na kuandamwa na maafisa usalama wa serikali, ambao wamekuwa wakimsaka kwa udi na uvumba tangu aukimbie mji mkuu Juba zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2016 09:25 UTC
  • Dak: Machar ametoroka Sudan Kusini kwa kuandamwa na maafisa usalama

Msemaji wa kiongozi wa upinzani nchini Sudan Kusini amesema Riek Machar ameikimbia nchi hiyo kutokana na kuandamwa na maafisa usalama wa serikali, ambao wamekuwa wakimsaka kwa udi na uvumba tangu aukimbie mji mkuu Juba zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

James Gatdet Dak, msemaji wa Machar amesema kiongozi huyo wa upinzani kwa sasa yuko katika mojawapo ya nchi za eneo hilo, ingawa hajafichua taifa linalomhifadhi makamu huyo wa rais aliyepigwa kalamu baada ya kuukimbia mji mkuu.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Dak ameongeza kuwa Machar anauguza jeraha la mguu kutokana na kutembea mwendo mrefu katika misitu ya nchi hiyo akiwakwepa  maafisa usalama waliokuwa wakimuandama. Hata hivyo serikali ya Juba imekanusha madai kuwa vyombo vya usalama vimekuwa vikimsaka Riek Machar, aliyeukimbia mji wa Juba baada ya kushadidi mapigano kati ya askari wanaomuunga mkono na wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir, ambapo watu zaidi ya 300 waliuawa.

Haya yanajiri siku moja baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Taban Deng Gai kumlaumu Machar kuwa amevuruga mchakato wa amani na kukiuka makubaliano ya kusitisha machafuko ya miezi kadhaa katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini akizungumza mjini Nairobi

Deng Gai aliyesema hayo mjini Nairobi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kusisitiza kuwa, yuko tayari kumuachia Machar wadhifa huo iwapo atarejea Juba.