Amnesty International: Serikali ya Uganda inatumia mbinu za mateso kuwatishia wapinzani
-
Amnesty International: Serikali ya Uganda inatumia mbinu za mateso kuwatishia wapinzani
Shirika la kimataifa la haki za binadamu, Amnesty International, limetangaza kuwa, vikosi vya usalama nchini Uganda vinatumia njia za mateso na ukamataji usio wa kisheria kuwatisha wapinzani kuelekea uchaguzi mkuu katikati ya mwezi huu wa Januari.
Shirika hilo la Msamaha Duniani linasema limekusanya ushahidi unaoonesha maafisa usalama wakiwapiga na kutumia gesi za machozi dhidi ya wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha NUP kinachoongozwa na Robery Kyagulani maarufu kama Bob Wine.
Ripoti ya Amnesty imetolewa wakati huu mkurugenzi wa mamlaka ya mawasiliano nchini Uganda, Nyombi Thembo, akikanusha madai kuwa watazima mtandao siku ya uchaguzi.
Kauli yake imekuja huku wizara ya mawasiliano ikionya vyombo vya Habari vitakavyorusha maudhui ya vurugu kuelekea na siku ya uchaguzi.
Hivi karibuni pia, Umoja wa Mataifa ulikosoa kuongezeka ukandamizaji dhidi ya upinzani na vyombo vya habari nchini Uganda kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi huu na kutaka uchunguzi ufanyike bila upendeleo kuhusu madai ya kukamatwa raia kiholela, kutoweka na "mateso".
Akiwa na umri wa miaka 81, Museveni anawania kuchaguliwa tena akibeba bendera ya chama tawala cha National Resistance Movement, NRM baada ya kuweko madarakani kwa karibu miaka 40.
Mwaka 2017, Bunge la Uganda liliondoa ukomo wa umri wa kikatiba wa kuwania urais, na hivyo kutoa mwanya kwa Museveni kugombea kwa muda wowote anaotaka.
Mshindani wake mkuu Bobi Wine amejenga matumaini ya mabadiliko nchini humo. Mwimbaji huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita wa urais mnamo 2021, kwa kupata 35% ya kura
Wine alidai ushindi wake uliibwa kupitia ujazo wa kura na makosa mengine. Hata hivyo tume ya uchaguzi wa Uganda ilikanusha madai hayo.