AU; Uchaguzi Somalia lazima ufanyike kama ilivyopangwa
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia amesiistiza juu ya azma ya umoja huo ya kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Rais na Bunge huko Somalia unafanyika kama ilivyoainishwa.
Francesco Madeira ameongeza kuwa uchaguzi wa Rais na Bunge nchini Somalia umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Septemba na mwanzoni mwa Oktoba kwa kushiriki taasisi zote za usalama za nchi hiyo. Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Afrika amesisitiza kwamba kufanyika uchaguzi huo si tu ni kwa ajili ya maslhi ya Somalia pekee, bali pia ni ushindi kwa nchi za eneo na taasisi za kimataifa. Madeira ameongeza kuwa, hadi sasa yamepatikana mafanikio mengi katika ushirikiano wa vikosi vya Somalia na askari wa Umoja wa Afrika mbele ya vitisho vya wanamgambo wa kundi la al Shabab, tangu kuwasili nchini humo askari huo wanaotekeleza majukumu yao kwa usimamizi wa Umoja wa Afrika AU.
Wakati huo huo Omar Mohamed Abdulle Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Somalia amebainisha kuwa uchaguzi wa Rais na Bunge wa nchi hiyo utafanyika kama ilivyopangwa yaani tarehe 30 Oktoba. Abdulle amewatolea wito shakhsia wa kisiasa wa Somalia na vile vile taasisi za kimataifa kufanya jitihada ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani.