WFP: Watu milioni 4.5 wanahitaji msaada wa chakula kaskazini mashariki mwa Nigeria
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa tangu mwezi Machi mwaka huu hadi sasa, idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula kaskazini mashariki mwa Nigeria imeongezeka maradufu na kufikia milioni 4.5.
Hayo ni kwa mujibu wa uhakiki uliofanywa na mashirika mbalimbali likiwemo la umoja huo la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Mkurugenzi wa WFP katika kanda ya Afrika Magharibi Abdou Dieng amesema ishara zote zinaonyesha kuwa hali inaelekea kuwa mbaya mno.
Kwa mujibu wa uhakiki uliofanywa katika majimbo ya Borno,Yobe na Adamawa idadi ya watu wanaotaabika kukabiliana na uhaba mkubwa wa chakula na walio katika hali mbaya ya dharura ya kuhitajia chakula ili waweze kubaki hai imeongezeka mara nne tangu mwezi Machi mwaka huu na kupindukia milioni moja.
Mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika majimbo hayo yamesababisha watu kuhama makazi yao, kuvurugika mfumo wa maisha ya watu na kupelekea kuwepo uhaba mkubwa wa chakula.
Kwa mujibu wa Dieng maelfu ya watu wameuawa au kujeruhiwa nchini Nigeria na katika nchi jirani za Chad, Cameroon na Niger katika kipindi cha siku kadhaa tu zilizopita, hali inayoashiria kuwa mashambulio yanayofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram yataendelea kuwafanya watu wengi zaidi wakabiliwe na baa la njaa na mateso.
Inakadiriwa pia kuwa kuna watu wasiopungua 65,000 katika maeneo mapya yaliyokombolewa kutoka mikononi mwa kundi hilo lakini bado hawajaweza kufikiwa katika maeneo ya majimbo ya Borno na Yobe na wanakabiliwa na hali ya ukame.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limetangaza kuwa linahitaji dola milioni 52 ili liweze kuendelea kutoa misaada ya kuokoa maisha ya watu hadi mwishoni mwa mwaka huu katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria.../