ICC 'yahofia' kuhusu kujiondoa kwa Mali, Burkina Faso na Niger
-
Hofu ya ICC kuhusu kujiondoa Mali, Burkina Faso na Niger
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imeeleza wasiwasi wake kuhusu kujiondoa Mali, Burkina Faso na Niger kwenye mahakama hiyo, ikisema kunadhoofisha harakati za kimataifa za kutafuta haki.
ICC yenye makao yake makuu Hague huwafungulia mashtaka watu binafsi kwa makossa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Mataifa hayo matatu ya Afrika Magharibi yanayoongozwa na jeshi yalijiondoa katika mahakama hiyo mwaka jana, yakiitaja kuwa ni "chombo cha ukandamizaji wa ukoloni mamboleo kinachotumiwa na ubeberu."
Nchi hizo tatu wanachama wa zamani wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) ziliunda Muungano wa Mataifa ya Sahel mnamo 2024.
Baraza la Nchi Wanachama wa ICC, ambalo linawakilisha nchi zinazounda mahakama hiyo, limeeleza kusikitishwa na hatua hiyo.
Taarifa iliyotolewa na baraza hilo jana Jumatano ilisema nchi zinazojiondoa katika mahakama ya ICC "zinatishia kudhoofisha harakati za pamoja za kutekeleza uadilifu na juhudi za kimataifa za kuwawajibisha wanaotenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu".
Mahakama hiyo ina wanachama 125 kwa sasa lakini mataifa kadhaa makubwa yakiwemo China, India, Russia na Marekani pamoja na utawala haramu wa Israel hayajajiunga ya mahakama hiyo.