Aug 31, 2016 04:26 UTC
  • ZHRC: Polisi ya Zimbabwe imefanya ukatili dhidi ya wapinzani

Tume ya Haki za Binadamu ya Zimbabwe (ZHRC) imelilaumu jeshi la polisi la nchi hiyo kuwa limefanya ukatili na kukanyaga haki za wapinzani wa serikali wakati wa kuzima maandamano yao katika kipindi cha miezi miwili ya hivi karibuni.

Katika taarifa yake ya kwanza kuhusu maandamano hayo, tume hiyo imesema kuwa, uchunguzi umebaini kuwepo mwenendo usiofaa na wa kutumia mabavu wa maafisa wa polisi na imewataka wahanga wa vitendo hivyo kuwasilisha mashtaka.

Tume ya Haki za Binadamu ya Zimbabwe ambacho ni chombo huru cha kujitegemea kilichoundwa mwaka 2013 imesema, inasikitisha kwamba polisi imekiuka haki za msingi za wananchi kama inavyothibitishwa na ushahidi uliokusanywa. ZHRC imesisitiza kuwa, wasiwasi kuhusu masuala ya usalama haupaswi kutumiwa kama kisingizio cha kukandamiza waandamanaji na kwamba wananchi wanapaswa kulindwa na polisi na si kufanyiwa ukatili.

Makumi ya watu wametiwa nguvuni nchini Zimbabwe kufuatia maandamano yaliyofanyika Ijumaa iliyopita dhidi ya serikali ya Rais Robert Mugabe anayeitawala nchi hiyo tangu mwaka 1987.

Wapinzani wa serikali ya Mugabe

Wananchi wa Zimbabwe wamekuwa wakifanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kupinga hali mbaya ya uchumi, ukosefu wa ajira na kucheleweshwa mishahara ya wafanyakazi wa serikali.

Kambi ya upinzani imepanga kufanya maandamano zaidi siku Jumatano na Ijumaa ijayo dhidi ya serikali ya Mugabe.

Tags