Sudan Kusini yakubali askari wengine 4,000 wa kulinda amani wa UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14662-sudan_kusini_yakubali_askari_wengine_4_000_wa_kulinda_amani_wa_un
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ameafiki kutumwa askari wengine zaidi 4,000 wa kulinda amani baada ya kuwa awali alikataa kutumwa kikosi cha kieneo kwa madai kuwa ni ukiukwaji wa haki ya kujitawala nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2016 03:09 UTC
  • Sudan Kusini yakubali askari wengine 4,000 wa kulinda amani wa UN

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ameafiki kutumwa askari wengine zaidi 4,000 wa kulinda amani baada ya kuwa awali alikataa kutumwa kikosi cha kieneo kwa madai kuwa ni ukiukwaji wa haki ya kujitawala nchi hiyo.

Kiir alitoa tamko hilo Jumapili baada ya kukutana na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika mji mkuu, Juba.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Umoja wa Mataifa na serikali ya Juba ilisema kuwa, serikali ya mpito ya umoja wa taifa imeidhinisha kutumwa kikosi hicho kitakachokuwa pia na askari wa nchi za eneo.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa

Sudan Kusini ilishuhudia wimbi jipya la machafuko tokea Julai 8 wakati kulipojiri ufyatulianaji risasi karibu na Ikulu ya Rais mjini Juba wakati Kiir na makamau wa rais wakati huo, Riek Machar walipokuwa mkutanoni. Watu 300 waliuawa katika mapigano hayo. Nchi hiyo ambayo ilipata uhuru baada ya kujitenga na Sudan imekuwa ikishuhudia machafuko tokea wakati huo.

Hitilafu za kisiasa na kikabila zinatajwa kuwa sababu kuu za mapigano na mivutano ya mara kwa mara kati ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka na hasimu wake, Machar anayetoka kabila la Nuer.