Sep 11, 2016 04:33 UTC
  • Waasi wa Mai Mai waafiki kusitisha mashambulizi Kongo

Duru za kuaminika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo zimearifu kuwa baadhi ya waasi wa kundi la Mai-Mai wamekubali kusitisha mashambulizi ikatika eneo la Masisi mkoani Kivu ya Kaskazini.

Viongozi wa wanamgambo wa Mai-Mai na waasi wengine wanaobeba silaha wamekubaliana kuhusu kusitisha mashambulizi na kuondoa vizuizi katika njia za  raia wa eneo la Masisi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Makubaliano hayo yalifikiwa tarehe 23 mwezi Agosti mwaka huu kati ya makundi yanayobeba silaha kwa jina la Muungano kwa Ajili ya Kongo Iliyo Huru  na waasi wa Mai-Mai. Wanamgambo hao wa Mai-Mai  wamejisalimisha kwa viongozi wa eneo la Masisi katika fremu ya makubaliano hayo, eneo linalopatikana katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wakati huo huo Jumuiya ya Kiraia katika mkoa wa Katanga hivi karibuni iliwataka wakazi wa mji wa Kalemie makao makuu ya mkoa huo wafanye mgomo wa wote katika kulalamikia ukosefu wa amani katika mji huo. Wakazi wa mji wa Kalemie walitolewa wito wa kufanya mgomo ili kulalamikia mauaji ya raia wawili yaliyofanywa na wavamizi wenye silaha wasiojulikana katika mji huo. Mauaji na hali ya ukosefu wa usalama vilivyoshuhudiwa katika siku za hivi karibuni katika mji wa Kalemie na katika maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo, yameibua hasira na malalamiko ya wakazi wa maeneo hayo. Kwa msingi huo hivi sasa kuna matarajio ya kurejea amani na uthabiti mashariki mwa Kongo baada ya   wanamgambo kadhaa wa kundi la Mai-Mai kukubali kusimamisha mashambulizi na hujuma za uharibifu dhidi ya raia wa eneo la Masisi mkoani Kivu ya Kaskazini.

Hasa ikizingatiwa kwamba  mazungumzo ya kitaifa kati ya wawakilishi wa serikali, vyama vya upinzani na makundi ya kiraia ya Kongo yameanza huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu tarehe Mosi mwezi huu. Tukio hili muhimu lenye lengo la kuzuia machafuko ya kisiasa huko Kongo tayari limeanza na litadumu kwa muda usiopungua wiki mbili. Sababu kuu iliyoshadidisha mgogoro wa kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni kuwepo wasiwasi kwamba  Rais Joseph Kabila ataongeza muda ili aweze kusalia madarakani na jitihada zake za kuifanyia marekebisho katiba ya Kongo ili kufanikisha suala hilo. Weledi wa mambo pia wanasema huenda Rais Joseph Kabila naye  kama walivyofanya Marais wengine kama Paul Kagme wa Rwanda na Denis Sasssou Nguesso wa Jamhuri ya Kongo akaifanyia marekebisho katiba ya Kongo DR  ili agombee tena kiti cha urais kwa muhula wa tatu.

Hii ni katika hali ambayo vyama vya upinzani na taasisi za kiraia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vinamtaka Rais Kabila ang'atuke madarakani  ifikapo Disemba 20 mwaka huu; muda ambao duru yake ya pili ya urais itamalizika.

Rais Joseph Kabila wa Kongo ambaye wapinzani wamemkalia kooni wakimtaka ang'atuke madarakani muda wake ukimalizika

Pamoja na hayo yote, majaji wa Mahakama Kuu ya Kongo wamemruhusu Rais Kabila kuendelea kusalia madarakani  madhali uchaguzi mpya wa rais haujafanyika nchini humo. Kwa msingi huo, weledi wa mambo wanaamini kuwa uchaguzi wa Rais wa Kongo  utafanyika mwaka 2018 au 2019, licha ya vizuizi na mikwamo inayowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo katika kuwaandikisha raia waliotimiza masharti ya kupiga kura.

Edem Kodjo Msuluhishi wa Umoja wa Afrika (AU) katika mgogoro wa Kongo na Waziri Mkuu wa zamani wa Togo amesisitiza kwenye ufunguzi wa kikao cha mazungumzo ya kitaifa ya Kongo kuwa, pande za nchi hiyo zinapasa kufikia mapatano ya mwisho kuhusu suala la kuendesha uchaguzi. 

Edem Kodjo Msuluhishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa kisiasa wa Kongo DR

Naye Vital Kamerhe Mjumbe wa vyama wa upinzani katika mazungumzo hayo ya kitaifa pia amebainisha kuwa demokrasia ni njia pekee inayoweza kuisaidia Kongo kujiondoa kwenye mgogoro na kwamba njia nyingine ghairi ya hiyo itakuwa ni kuirejesha nchi hiyo kwenye machafuko.

 

 

Tags