Waalgeria waandamana kulalamikia kuwekwa jina la Israel katika kitabu cha masomo
Raia wa Algeria wamefanya maandmano kulalamikia hatua ya kuandikwa jina la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel mahala pa jina la Palestina katika kitabu cha kufundishia nchini humo.
Abdul-Razzaq Qasum, mkuu wa jumuiya ya maulama wa Kiislamu nchini Algeria sanjari na kuitaja hatua hiyo kama kosa kubwa la kihistoria amesema kuwa, lengo la kuandikwa jina la utawala wa Kizayuni katika kitabu cha kufundishia ni kujaribu kuboresha uhusiano wa kielimu na Israel. Amesisitiza kuwa, kuingizwa katika akili za watoto wadogo wa Algeria jina la utawala huo katili, ni kitu hatari sana.
Naye Ahmad Khalid, mkuu wa jumuiya ya wazazi wa wanafunzi nchini Algeria amekosoa vikali hatua hiyo ya serikali ya Algiers na kusema kuwa, kitendo hicho ni kosa kubwa sana ambalo wahusika wake wanatakiwa kuchukuliwa adhabu kali. Kufuatia hali hiyo sambamba na kuendelea malalamiko ya kulaani hatua ya kuandikwa jina la utawala haramu wa Kizayuni mahala pa jina la Palestina katika kitabu cha kufundishia, viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo nchini humo, wameamua kukusanya vitabu hivyo kwa ajili ya kuvifanyia marekebisho.
Katika hatua nyingine Wizara ya Elimu na Mafunzo nchini Algeria imetangaza kuanzisha uchunguzi wa kisheria kutokana na kosa hilo lililojitokeza. Kwa mujibu wa wizara hiyo, serikali ya nchi hiyo imeahidi kuheshimu masuala nyeti kama vile kutoutambua utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kadhalika, au mahusiano na Sahara Magharibi na mfano wa hayo.