Hatima ya Mugabe kutolewa madarakani na mahakama ya katiba Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17002-hatima_ya_mugabe_kutolewa_madarakani_na_mahakama_ya_katiba_zimbabwe
Hatima ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye ameiongoza nchi hiyo tangu ijinyakulie uhuru sasa ipo mikononi mwa mahakama ya katiba ya nchi hiyo.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Oct 08, 2016 10:35 UTC
  • Hatima ya Mugabe kutolewa madarakani na mahakama ya katiba Zimbabwe

Hatima ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye ameiongoza nchi hiyo tangu ijinyakulie uhuru sasa ipo mikononi mwa mahakama ya katiba ya nchi hiyo.

Chama cha upinzani cha MDC kimesema kimelazimika kupeleka hoja ya kutokuwa na imani na Rais Mugabe katika mahakama ya kariba baada ya bunge la nchi hiyo kushindwa kuijadili.

James Maridadi, mbunge wa chama cha MDC amesema ni wazi kwamba Spika wa bunge hilo Jacob Mudenda ameshinikizwa kutoiwasilisha hoja hiyo bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, ikizingatiwa kuwa alipewa ilani ya hoja hiyo tangu mwezi Julai mwaka huu.

Mbunge huyo amesema tayari amewaagiza mawakili wake kuipa bunge notisi kuhusu hoja hiyo ya kutokuwa na imani na Rais Mugabe kufikishwa katika mahakama ya katiba, akisisitiza kuwa haki yake ya uakilishi imekanyagwa na mhimili muhimu wa serikali (bunge) na ndiposa amelazimika kuelekea kotini kutafuta haki.

Maandamano ya wapinzani Zimbabwe

Hii ni katika hali ambayo, katika wiki za hivi karibuni, Zimbabwe imeshuhudia maandamano ya wapinzani wanaomtaka Rais Mugabe aondoke madarakani wakisisitiza kuwa ameshindwa kutatua matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira nchini humo.

Mugabe, mwenye umri wa miaka 92 na ambaye ametawala Zimbabwe tokea ipata uhuru wake mwaka 1980 ametangaza kuwa atatetea kiti chake katika uchaguzi mkuu  wa mwaka 2018.