Oct 12, 2016 15:55 UTC
  • Bunge la Burundi lapasisha muswada wa kujiondoa mahakama ya ICC

Bunge la Burundi leo limepasisha muswada wa kujiondoa nchi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) baada ya Umoja wa Mataifa kuanza kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika nchini humo.

Muswada huo umepasishwa kwa kura 94 za ndiyo, mbili za kupinga na wabunge 14 hawakupiga kura. Baada ya kupasishwa na Bunge, sasa muswada huo utapelekwa katika Baraza la Seneti ya nchi hiyo kabla ya kupasishwa na Rais Pierre Nkurunziza.

Mwezi Aprili mwaka huu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama ya kimataifa ya ICC, Fatou Bensouda alitangaza kuwa, ataanzisha uchunguzi wa awali kuhusiana na vitendo vya ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni hatua ya kwanza ya kufungua kesi juu ya madai ya mauaji ya raia, mateso na vitendo vya kubakwa na kunajisiwa wafuasi wa kambi ya upinzani dhidi ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.

Raia waliojerehiwa kwa kupigwa na kuteswa na jeshi la Burundi

Wiki mbili zilizopita pia Umoja wa Mataifa Umoja wa Mataifa ulizinduliwa uchunguzi kuhusu ukiukwaji wa haki nchini Burundi baada ya ripoti kutahadharisha juu ya uwezekano wa kufanyika uhalifu dhidi ya binadamu na hatari ya kutokea mauaji ya kimbari.

Jana Jumanne pia serikali ya Burundi ilitangaza kuwa, imesimamisha ushirikiano wake na Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa madai kuwa imeshiriki katika kutayarisha ripoti iliyodai kuwa ni ya urongo dhidi ya serikali ya Bujumbura.

Wapinzani wa serikali ya Rais Nkurunziza

Mgogoro wa Burundi ulizuka mwanzoni mwa mwaka jana, kufuatia uamuzi wa chama tawala CNDD-FDD kumuidhinisha Pierre Nkurunziza kugombea urais wa nchi hiyo kwa muhula wa tatu mfululizo katika uchaguzi uliopita. Wapinzani wa serikali wanasema uamuzi huo ulikiuka makubaliano ya amani ya Arusha na katiba ya Burundi.

 

Tags