Machar: Nataka kukutana na Rais Zuma wa Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17581-machar_nataka_kukutana_na_rais_zuma_wa_afrika_kusini
Makamu wa rais wa zamani na kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini amesema anataka kuonana ana kwa ana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ili amueleze 'mambo nyeti' juu ya mgogoro wa kisiasa na mapigano yanayoendelea katika nchi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2016 00:59 UTC
  • Machar: Nataka kukutana na Rais Zuma wa Afrika Kusini

Makamu wa rais wa zamani na kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini amesema anataka kuonana ana kwa ana na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ili amueleze 'mambo nyeti' juu ya mgogoro wa kisiasa na mapigano yanayoendelea katika nchi yake.

Katika mahojiano na jarida la News24 la Afrika Kusini, Riek Machar amesema serikali ya Afrika Kusini inafaa kuwa mstari wa mbele mara tu duru mpya ya mazungumzo ya amani itakapoanza akisisitiza kuwa, mgogoro wa Sudan Kusini unahitajia mchakato wa kisiasa ili kuupatia ufumbuzi.

Machar ambaye aliwasili nchini Afrika Kusini wiki hii akitokea Khartoum kwa ajili ya 'uchunguzi wa kiafya' amesema Rais Zuma na makamu wake Cyril Ramaphosa wana wajibu wa kisiasa wa kumsikiliza kuhusu hali ya kisiasa na kiusalama nchini mwake.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

Akizungumza siku chache zilizopita katika ziara yake nchini Kenya, Rais Zuma alinukuliwa akiikosoa harakati ya SPLM kwa kuanzisha uasi dhidi ya serikali mjini Juba na kutoa wito akimtaka Machar arejee nchini mwake kwa ajili ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro uliopo.

Hivi karibuni, Machar aidha alimwomba Katibu Mkuu mteule wa Umoja wa Mataifa António Guterres kufanya juhudi za kukomesha vita vya ndani katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Katika barua yake kwa Guterres, Machar alibainisha kuwa Agosti mwaka 2015, pande zinazopigana nchini Sudan Kusini zilisaini hati ya makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kutatua mgogoro uliopo, lakini hati hiyo ilikiukwa kwa kuanza tena mapigano mnamo mwezi Julai mwaka huu, ambapo makumi ya watu waliuawa na makumi ya maelfu ya wengine kuwa wakimbizi.