Afrika Kusini kujiondoa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17866-afrika_kusini_kujiondoa_mahakama_ya_kimataifa_ya_jinai_icc
Afrika Kusini imetangaza rasmi azma yake ya kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 21, 2016 10:12 UTC
  • Afrika Kusini kujiondoa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC

Afrika Kusini imetangaza rasmi azma yake ya kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Maite Nkoana-Mashabane, Waziri wa Mashauri ya Kigeni amesema nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imeiandikia barua ya ilani ICC, ikiieleza azma yake ya kujiondoa kwenye uanachama wa mahakama hiyo iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi, kwa msingi kuwa sheria zake haziendani na majukumu ya mahakama hiyo.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

Naye Michael Masutha, Waziri wa Sheiria wa Afrika Kusini amesema nchi hiyo imelazimika kuanzisha mchakato wa kujiondoa ICC, kwa kuwa majukumu ya mahakama hiyo ya kimataifa hayauwiani na sheria za nchi hiyo, zinazowapa kinga ya kidiplomasia viongozi walio madarakani.

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi kusaini mkataba wa kujiondoa nchi yake katika Makahama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Tarehe 12 mwezi huu wa Oktoba, bunge la Burundi lilipasisha muswada wa kujiondoa nchi hiyo katika mahakama ya ICC.

Nchi kadhaa za Kiafrika zimetishia kujiondoa kwenye mahakama hiyo kutokana na hatua yake ya kuendelea kuwasakama viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na mataifa ya Magharibi.