Zaidi ya watoto 100 wanaotumika vitani Sudan Kusini wakombolewa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18220-zaidi_ya_watoto_100_wanaotumika_vitani_sudan_kusini_wakombolewa
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza habari ya kukombolewa zaidi ya watoto wadogo 100 waliokuwa wanatumika vitani nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 27, 2016 05:29 UTC
  • Zaidi ya watoto 100 wanaotumika vitani Sudan Kusini wakombolewa

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza habari ya kukombolewa zaidi ya watoto wadogo 100 waliokuwa wanatumika vitani nchini Sudan Kusini.

Mahimbo Mdoe, mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Kusini amenukuliwa na vyombo vya habari akitangaza habari hiyo na kufafanua kwa kusema, watoto wadogo 145 waliokuwa wanatumiwa na makundi mawili yenye silaha; lile la Riek Machar, mkuu wa waasi wa Sudan Kusini na lile la Cobra, katika mji wa Pibor huko mashariki mwa Sudan Kusini, wamekombolewa. Kundi la Cobra ni lile kundi la waasi lililowahi kutiliana saini makublaiano ya amani na serikali ya Sudan Kusini mwaka 2014.

Ameongeza kuwa, watoto hao 145 wamepokonywa silaha na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa afya zao na kuandikishwa majina yao katika mpango maalumu wa shirika hilo, watapewa nguo za kiraia. Baada ya hapo watarudishwa kwa familia zao na wataendelea kupewa msaada wa chakula kwa muda wa miezi mitatu.

 

Mwakilishi huyo wa UNICEF nchini Sudan Kusini amebainisha pia kuwa, shirika hilo litaendelea na mpango wake wa kukomboa watoto zaidi wanaotumika vitani. Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, kuna watoto wadogo 16 elfu wanaotumika vitani nchini Sudan Kusini.

Mahimbo Mdoe amesema pia kuwa, lengo la UNICEF ni kuhakikisha kuwa watoto hao wanarudi mashuleni na kuandaliwa kwa ajili ya kuwa watumishi wazuri wa jamii zao watakapofika ukubwani.