Nov 13, 2016 08:10 UTC
  • Tunisia yakadhibisha madai ya kuwepo kambi ya kijeshi ya Marekani nchini humo

Waziri Mkuu wa Tunisia, Youssef Chahed amekadhibisha habari za kuwepo kambi ya kijeshi ya Marekani na ghala la silaha la Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) nchini humo.

Kwa mujibu wa Youssef Chahed, ushirikiano wa kijeshi uliopo baina ya Tunisia na Marekani, unahusu tu masuala ya kiufundi, kiteknolojia, kubadilishana uzoefu kwa ajili ya kulinda mipaka na kununua silaha za kisasa za kijeshi. Chahed amekadhibisha madai ya gazeti la Washington Post juu ya kupaa ndege zisizo na rubani za jeshi la Marekani kutoka ardhi ya Tunisia na kuongeza kuwa, hadi sasa ndege za aina hiyo hazijawahi kuruka kutokea ardhi ya nchi yake kwenda Libya au Algeria.

Ndege isiyo na rubari ya Marekani

Pamoja na serikali ya Tunis kukadhibisha habari za kuepo kambi hiyo ya kijeshi ya Marekani nchini humo, lakini ushahidi unaonyesha kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imekusudia kujenga kambi ya aina hiyo kwa ajili ya ndege zake zisizo na rubani barani Afrika hususan katika eneo la kaskazini mwa bara hilo. Ukweli ni kwamba hivi sasa Washington kwa kutumia kisingizio cha harakati za makundi ya kigaidi na kiwahabi kama Daesh (ISIS) huko Libya, Boko Haram nchini Nigeria na nchi jirani, ash-Shabab nchini Somalia na makundi mengine madogomadogo yenye mfungamano na genge la kigaidi la al-Qaidah katika nchi za kaskazini mwa Afrika na eneo la Jangwa la Sahara, inakusudia kujipanua kijeshi, ikiwa ni pamoja na kujenga kambi ya jeshi ya ndege zisizo na rubani katika maeneo hayo. Katika miaka ya hivi karibuni Marekani imekuwa ikilipa uzito bara la Afrika kwa malengo maalumu na imeanzisha kikosi cha jeshi kilichopewa jina la AFRICOM.

Askari wa Marekani akiongoza moja ya ndege zisizo na rubani huko Afrika

Amri ya kuanzishwa kikosi hicho ilitolewa mwezi Oktoba mwaka 2007 na rais wa wakati huo wa Marekani, George W. Bush na kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2008 yaani mwaka mmoja baadaye, kulianzishwa rasmi operesheni za jeshi za nchi hiyo barani Afrika chini ya kikosi hicho. Kuundwa kikosi hicho cha AFRICOM kunaonesha ni kwa kiasi gani viongozi wa Marekani wanavyofuatilia malengo ya kistratijia barani Afrika, hususan kwa kuzingatia juhudi zinazofanywa na madola makubwa kwa ajili ya kujikita zaidi barani humo. Kwa mtazamo wa viongozi wa usalama na kijeshi nchini Marekani, uwepo wa kijeshi wa nchi hiyo barani Afrika unadhamini maslahi yake kama ambavyo pia ni hatua moja mbele kwa ajili ya kukabiliana na madola mengine kama vile Uchina. Harakati hiyo inatekelezwa na Washington kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Kwa mtazamo wa Marekani, bara la Afrika linaelekea kwenye hali ya kuwa ngome ya makundi ya kigaidi na kufurutu mipaka.

Moja ya viwanja vya ndege za kijeshi vinavyotumiwa na askari wa Marekani nje ya miapaka ya nchi hiyo

Kama tulivyosema , harakati za makundi kama Daesh, al-Qaidah, Boko Haram, ash-Shabab katika nchi za bara hilo, ndizo zinazotumiwa kama kisingizio na madola ya Wamagharibi kujizatiti barani humo. Hivi sasa Marekani inatumia ndege zisizo na rubani katika operesheni zake za kufanya upelelezi na mashambulizi ya anga katika nchi husika. Baada ya kushindwa kukubwa katika mashambulizi yake nchini Afghanistan na Iraq ambako kumeenda sambamba na kuongezeka kwa ugaidi hata katika nchi za Magharibi na Asia Washington imeamua kuelekeza stratijia yake barani Afrika sanjari kabisa na kutenga kiasi kikubwa fedha na kutayarisha idadi kubwa ya jeshi kwa ajili ya kufanikisha mpango huo. Aidha kuongezeka wimbi la uharamia huko katika eneo la Pembe ya Afrika, machafuko yanayoshuhudiwa katika nchi kadhaa na pia kupanuka kwa harakati za magenge ya kigaidi ni kati ya mambo ambayo yanatumwia kama kisingizio cha Washington kuendelea kujitanua barani Afrika.

Kwa kuzingatia ushirikiano wa kijeshi uliopo baina ya Tunisia na Marekani na pia umuhimu iliyonayo nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika kama ngome ya kuendesha harakati za ujasusi na mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la Daesh, na licha ya serikali ya Tunis kukadhibisha ripoti ya gazeti la Washington Post, lakini haiwezi kukadhibisha ukweli kwamba, Pentagon inafanya njama za kuanzisha kambi ya kijeshi kwa ajili ya ndege zake zisizo na rubani ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Tags