Daesh wachinja wanazuoni wawili wa Kisuni nchini Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19891-daesh_wachinja_wanazuoni_wawili_wa_kisuni_nchini_misri
Hisia tofauti zimeendelea kutolewa kwenye mitandao ya kijamii baada ya wafuasi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS kusambaza picha za wanazuoni wawili wa Kisuni waliowachinja kwa kuwakata vichwa katika eneo la Sinai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 21, 2016 04:11 UTC
  • Daesh wachinja wanazuoni wawili wa Kisuni nchini Misri

Hisia tofauti zimeendelea kutolewa kwenye mitandao ya kijamii baada ya wafuasi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS kusambaza picha za wanazuoni wawili wa Kisuni waliowachinja kwa kuwakata vichwa katika eneo la Sinai.

Mtandao wa habari wa News24 umeripoti habari hiiyo na kuongeza kuwa, mmoja kati ya wanazuoni hao wawili wa Kisunni waliokatwa vichwa na Daesh ni mwanachuoni kipofu aliyetambulika kwa jina la Sheikh Suleiman Abu Heraz, ambaye alitekwa nyara na wakufurishaji hao nyumbani kwake huko al-Arish, wiki mbili zilizopita. Mwanachuoni wa pili Kisunni ambaye wakaazi wa eneo hilo wamesema kuwa ni mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu katika Peninsula ya Sinai nchini Misri na ambaye amechinjwa kwa kukatwa kichwa na genge la kigaidi la Daesh ni Sheikh Said Abdel-Fattah, aliyetekwa nyara na matakfiri hao mwezi mmoja uliopita.

Daesh wakiendeleza jinai zao eneo la Sinai

Mapema mwezi huu, mahakama moja nchini Misri iliwahukumu kifo watu wawili kwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi. Iliarifiwa kuwa, wawili hao pamoja na wengine 12 waliohukumiwa vifungo tofauti walijiunga na magenge yenye misimamo mikali nchini Libya na walitiwa mbaroni wakati walipokuwa njiani kurejea nchini Misri.

Ikumbukwe kuwa, tangu miaka miwili nyuma hadi hivi sasa, watu wenye silaha wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kuvizia dhidi ya raia, viongozi na maafisa wa kulinda usalama pamoja na vituo vya kijeshi na vya polisi katika maeneo tofauti ya Misri hususan kwenye mkoa wa Sinai Kaskazini na wameshaua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.