Nov 23, 2016 08:16 UTC
  • Tanzania mwenyeji wa mkutano wa AU kuhusu demokrasia na haki

Duru ya tano ya mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Afrika kuhusu Demokrasia, Haki, za Binadamu na Uongozi imeanza hii leo mjini Arusha Tanzania.

Mkutano huo ambao unatazamiwa kumalizika Novemba 26, umefunguliwa rasmi na Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanza kazi Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, maadhimisho ya miaka 13 ya Protokali ya Maputo kuhusu Haki za Wanawake na miaka 15 ya Kamati ya Wataalamu wa Nchi za Afrika kuhusu Haki na Maslahi ya Watoto.

Wakuu wa AU

Aidha mkutano huo wa Arusha utaangazia hatua zilizopigwa na Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyoundwa miaka 29 iliyopita sambamba na mafanikio ya miaka 35 tangu kusainiwa Hati ya Haki za Binadamu barani Afrika.

Itakumbukwa kuwa, Umoja wa Afrika ulitangaza kuwa 2016 utakuwa Mwaka wa Haki za Binadamu barani Afrika na hususan haki za wanawake.

Wajumbe zaidi ya 300 wakiwemo wawakilishi wa nchi wanachama wa AU, wasomi, watafiti, asasi za kiraia, waandishi wa habari, vijana na washirika wa kimataifa wanahudhuria mkutano huo wa Arusha.

Tags