Jeshi la Sudan Kusini lakadhibisha tuhuma za Human Rights Watch
Jeshi la Sudan Kusini limekadhibisha tuhuma zilizotolewa na shirika la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch juu ya kufanya jinai dhidi ya binaadamu.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Lul Ruai imekadhibisha tuhuma hizo za kutenda jinai za kivita dhidi ya raia na kulitaka shirika hilo kuthibitisha madai hayo. Ruai amesema, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo kwa kuwahoji raia wa mji wa Yei, jinai hizo zilifanywa na waasi wanaomuunga mkono Riek Machar, makamu wa rais wa zamani aliyeuzuliwa na Rais Salva Kiir.
Kadhalika Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amesema kuwa, ni hivi karibuni tu waasi hao wametekeleza mauaji dhidi ya watu 21 katika mji ulio katikati ya Juba na Yei, ambapo mbali na mauaji, waasi hao wenye silaha waliteketeza kwa moto magari kadhaa na kuwabaka wanawake.
Jumatano iliyopita, Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International lilitoa ripoti mpya ambayo ililituhumu jeshi la serikali na waasi wenye silaha kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni.
Wakati huo huo habari za hivi punde zimeripoti kujiri mauaji ya watu 25 na wengine 17 kujeruhiwa, katika mfululizo wa mashambulizi ya kundi moja lililojitenga na lenya mafungamano na Riek Macha, huko mashariki mwa Sudan Kusini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo wakazi wa eneo hilo wamepatwa na wasi wasi mkubwa na kuwafanya kukimbia nyumba zao.