UN yatoa wito wa kusaidiwa nchi ya Somalia
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa jumuiya za kitaifa kutoa misaada ya kibinadamu kwa Somalia.
Mratibu wa Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Peter de Clercq amezitaka jumuiya za kimataifa kulipa kipaumbele suala la kupeleka misaada ya kibinadamu nchini Somalia akisisitiza kuwa, Wasomali wanasumbuliwa na ukame wa muda mrefu na wanahitaji misaada ya dharura.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hali ya familia maskini nchini Somalia inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Peter de Clercq ameongeza kuwa, muda unazidi kupita na kwamba jumuiya za misaada ya kibinadamu zinahitaji fedha zaidi kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro wa ukame na matatizo mengine yanayotokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la al Shabab.
Awali Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, umepokea asilimia 47 tu kati ya dola milioni 885 zinazohitajika kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya msingi ya Wasomali wanaosumbuliwa na njaa na ukosefu wa maji.
Ripoti ya umoja huo pia inasema kuwa watoto laki 3 na 20 elfu wenye umri wa chini ya miaka mitano wanasumbuliwa na lishe dunia nchini Somalia.