Tunisia yasambaratisha makundi 160 ya magaidi
Vikosi vya usalama Tunisia vimefanikiwa kusambaratisha makundi 160 ya kigaidi nchini humo katika miezi 10 ya kwanza ya mwaka huu.
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imesema magaidi waliokamatwa katika kipindi hicho cha Januari hadi Oktoba mwaka huu ni 850 ikilinganishwa na 547 mwaka wote wa 2015.
Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini iliimarisha oparesheni za kuwakamata magaidi baad aya kushuhudia hujuma kadhaa za kigaidi mwaka jana ambapo idadi kubwa ya watu waliuawa wakiwemo watalii.
Mwezi Machi mwaka huu, vikosi vya usalama vya Tunisia vilizuia hujuma ya magaidi wa ISIS au Daesh ambao walikuwa wamelenga kuuteka mji wa Ben Guerdan karibu na mpaka wa nchi hiyo na Libya.
Tunisia ni kati ya nchi chache za Kiarabu ambazo zimefanikiwa kuwa na mfumo thabiti wa kidemokrasia baada ya mwamako wa wananchi ulioanza mwaka 2011 huku nchi jirani yake, yaani Libya ikiendelea kukumbwa na msukosuko mkubwa.