Tunisia: Ghannouchi na wenzake wahukumiwa kifungo cha maisha jela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138860-tunisia_ghannouchi_na_wenzake_wahukumiwa_kifungo_cha_maisha_jela
Mahakama ya Tunisia imemhukumu kifungo cha maisha jela kiongozi wa Harakati ya Ennahdha na Spika wa zamani wa Bunge, Rached Ghannouchi (miaka 84), pamoja na kuwahukumu wenzake katika kesi inayojulikana kwa jina la "Ennahdha Movement's Secret Apparatus".
(last modified 2026-06-03T13:24:09+00:00 )
Jun 03, 2026 13:16 UTC
  • Rached Ghannouchi
    Rached Ghannouchi

Mahakama ya Tunisia imemhukumu kifungo cha maisha jela kiongozi wa Harakati ya Ennahdha na Spika wa zamani wa Bunge, Rached Ghannouchi (miaka 84), pamoja na kuwahukumu wenzake katika kesi inayojulikana kwa jina la "Ennahdha Movement's Secret Apparatus".

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Tunisia, "Tunis Afrique Presse," Chumba cha Jinai kinachojishughulisha na kesi za ugaidi katika Mahakama ya Mwanzo ya Tunis kimetoa hukumu zake, ambazo ni kati ya miaka 10 hadi kifungo cha maisha jela.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, mahakama imeamua kwamba washtakiwa wamepatikana na hatia ya "makosa ya kuunda kundi la kigaidi".

Hukumu hizo zinaanzia kifungo cha maisha jela na miaka 96 kwa Mustafa Khader hadi kifungo cha maisha jela na miaka 76 dhidi ya Reda Barouni, Taher Boubahri, Kamal Al-Aifi na washtakiwa wengine saba. Rached Ghannouchi pia amehukumiwa kifungo cha maisha pamoja na miaka 30 jela.

Kesi hii ilianzishwa mapema mwaka wa 2022 kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Mwendesha Mashtaka wa Umma na timu ya utetezi ya wanasiasa Chokri Belaid na Mohamed Brahmi, ambao waliuawa mnamo Februari na Julai 2013.

Timu ya utetezi wakati huo ilishutumu kile ilichokiita "chombo cha siri cha Ennahda" kwa kuhusika katika mauaji hayo, na kwa "kufanya ujasusi na kuingilia taasisi za serikali."

Baadhi ya viongozi wa harakati hiyo, hasa Rached Ghannouchi, walituhumiiwa kuendesha na kusimamia chombo hicho cha siri, ingawa harakati hiyo imekanusha tuhuma hizo na kuzitaja kuwa "za kisiasa".

Kabla ya hapo, Harakati ya Ennahda ya Tunisia ilitangaza kuwa afya ya kiongozi wake, Rashid Ghannouchi, imedhoofika zaidi gerezani na kwamba amehamishiwa hospitalini.  Ennahda imetaka kuachiliwa huru Ghannouchi na kufutwa hukumu zilizotolewa dhidi yake.

Vilevile chama cha upinzani cha National Salvation Front kimetaka Ghannouchi aachiliwe mara moja kutokana na hali yake ya kiafya kuwa mbaya.

Mnamo Aprili 17, 2023, askari usalama wa Tunisia walivamia nyumba ya Ghannouchi na kumkamata, kabla ya mahakama ya chini kuamuru afungwe kwa mashtaka ya kutoa kauli za "kuchochea machafuko na uasi."

Hata hivyo, vyama vya siasa vya Tunisia vinaamini kwamba hatua za kipekee zilizoanzishwa na Rais Kais Saied wa nchi hiyo mnamo Julai 2021 zinawakilisha "mapinduzi dhidi ya katiba na juhudi za kuimarisha utawala wa kidikteta."