Dec 12, 2016 02:39 UTC
  • Waislamu Nigeria wazidi kushinikizwa na serikali kwa kisingizio cha kuimarishwa usalama

Kufuatia kuongezeka hujuma za kigaidi nchini Nigeria, serikali ya Abuja inatumia kisingizio hicho kuwakadamiza wananchi hasa Waislamu.

Hivi karibuni kumejiri hujuma mbaya za kigaidi katika mji wa Madagali kaskazini mashariki mwa Nigeria. Yusuf Mohammad mkuu wa serikali ya manispa ya Madagali ametangaza kuwa waliopoteza maisha katika hujuma hiyo ya Ijumaa ni watu 56 huku wengine 177 wakijeruhiwa.

Mji wa Madagali uko umbali wa kilomita 276 kutoka mji wa Yola ambao mwaka 2014 ulikuwa moja ya miji ilkiyotekwa na kundi la kigaidi la Boko Haram na kukombolewa Machi 2015 kutoka mikononi mwa magaidi hao.

Badare Akintoye msemaji wa Jeshi la Nigeria amesema  kundi la kigaidi la Boko Haram ndilo lililotekeleza hujuma hiyo.

Ni wazi kuwa kushindwa jeshi la Nigeria kukabiliana na magaidi wa Boko Haram ndicho chanzo cha kupoteza maisha maelfu ya raia katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Hujuma za Boko Haram katika maeneo mbali mbali ya Nigeria zinaongezeka huku Kamanda wa Jeshi la Anga la Nigeria akiwa ametangaza kuwa vikosi vyote vya usalama nchini humo vinapaswa kushirikiana kuangamiza kundi la Boko Haram.

Hujuma ya kigaidi Nigeria

Sadique Abubakar Mkuu wa Jeshi la Anga la Nigeria ameashiria kuongezeka hujuma za Boko Haram na kusisitiza udharura wa kuwepo ushirikiano wa vikosi vyote vya jeshi la Nigeria kwa lengo la kuangamiza kundi hilo.

Tokea mwaka 2010 hadi sasa, magaidi wa Boko Haram wameua zaidi ya watu 13,000 nchini Nigeria na katika nchi jirani.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria katika taarifa kufuatia hujuma za hivi karibuni za kigaidi amesisitiza ulazima wa watu wa Nigeria kuwa waangalifu na kuwataka washirikiane na vikosi vya usalama katika vita dhidi ya ugaidi.

Kufuatia ongezeko la hujuma za kigaidi, utawala wa kipolisi umeenea kote Nigeria na wanajeshi wanaonekana katika miji yote huku hofu ikiwa imetanda mikononi mwa wananchi wa kawaida.

Aidha katika baadhi ya majimbo serikali imepiga marufuku mijumuiko na hivyo kuzidisha mashinikizo dhidi ya raia hasa Waislamu ambao huandaa mijumuiko mbali mbali ya kidini.

Haya yanajiri katika hali ambayo Waislamu nchini Nigeria wanasubiri serikali itekeleze amri ya mahakama kuu ya kumuahcilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaki, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ambaye yuko korokoroni kwa mwaka mmoja sasa pasina kufunguliwa mashtaka.

Baadhi ya duru zinadokeza kuwa, Sheikh Zakzaki na mke wake wamehamishwa kutoka eneo walilokuwa wakishikiliwa na kupelekwa kusikojulikana na vikosi vya usalama vya Nigeria.

Kwa mujibu wa hukumu ya Mahakama Kuu ya Kifedelari ya Nigeria, Sheikh Zakzaki na mke wake wanapaswa kuachiliwa huru lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kuhusiana na hujumu hiyo.

Magaidi wa Boko Haram

Waislamu nchini Nigeria wiki iliyopita  waliandamana wakitaka Sheikh Zakzaki aachiliwe huru mara moja.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeitaka serikali ya nchi hiyo kuheshimu harakati za kijamii na za kisheria za Waislamu. Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imekuwa ikifuata sera za amani na maelewano sambamba na kukosoa ukosefu wa uadilifu na ufisadi nchini humo na imekuwa ikiwatetea wananchi ili hali yao ya kimaisha iboreke.

Aidha katika uga wa kimataifa, harakati hiyo imekuwa ikikosoa sera za Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni kupitia maandamano ya mamilioni kaskazini mwa Nigeria.

Hivi sasa vita dhidi ya ugaidi ni kisingizio kinachotumiwa na vikosi vya usalama vya Nigeria kuwakadamiza wananchi na kuzidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu ikiwa ni pamoja na kuwawekea vizingiti katika harakati zao. Kwa msingi huo inatarajiwa kuwa katika siku za usoni tutashuhudia wimbi jipya la ukandamizwaji Waislamu wa Nigeria.

 

Tags