Iran na Afrika Kusini zasaini hati ya ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21403-iran_na_afrika_kusini_zasaini_hati_ya_ushirikiano_wa_kiulinzi_na_kijeshi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini zimetia saini hati ya maelewano ya ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 14, 2016 04:27 UTC
  • Iran na Afrika Kusini zasaini hati ya ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini zimetia saini hati ya maelewano ya ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi.

Hati hiyo imetiwa saini na Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Hossein Dehqan na mwenzake wa Afrika Kusini, Nosiviwe Noluthando Mapisa-Nqakula mjini Pretoria. 

Baada ya kutiwa saini hati hiyo ya maelewano ya ushirikiano wa kijeshi, mawaziri hao wawili wamezungumza na waandishi habari wakisisitiza udharura wa kuzidishwa ushirkiano wa kiulinzi na kijeshi kati ya nchi hizo mbili, kufanya jitihada za kuimarisha amani na usalama wa kikanda na kimataifa na kudumisha mapambano ya pande zote dhidi ya ugaidi.

Hati hiyo ya maelewano pia imetilia mkazo suala la ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za usalama wa baharini, masuala ya mafunzo na kubadilishana uzoefu katika medani ya kupambana na uhalifu wa kupangwa.

Brigedia Jenerali Hossein Dehqan 

Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Hossein Dehqan jana pia alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini. 

Katika mazungumzo hayo Rais Zuma alisema kuwa, Iran na Afrika Kusini ni nchi mbili muhimu na zinazojitawala na kwamba, Pretoria ina azma kubwa ya kupanua zaidi uhusiano na Iran na wala haitaruhusu upande wowote kuvuruga uhusiano huo.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi wa Iran ameashiria uhusiano wa miaka mingi wa Iran na chama cha ANC wakati wa mapambano yake dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na vilevile uhusiano wa kirafiki wa nchi hizo mbili katika miongo miwili iliyopita na kusema: Bara la Afrika lina nafasi maalumu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba, katika siasa zake, Tehran inalipa kipaumbele suala la kunyanyua juu kiwango cha uhusiano wake na Afrika Kusini.

Marais Jacob Zuma na Hassan Rouhani

Vilevile ameishukuru Afrika Kusini kutokana na misimamo yake kuhusu faili la nyuklia la Iran na safari iliyofanywa hivi karibuni na Rais Jacob Zuma nchini Iran na kusisitiza kuwa, safari hiyo ilikuwa chachu ya kuweko harakati kubwa zaidi katika ushirikiano wa nchi hizi mbili hususan katika masuala ya kiulinzi na kijeshi.