Kivuli cha mauti chawafunika maelfu ya watoto Afrika
(last modified Fri, 16 Dec 2016 14:44:24 GMT )
Dec 16, 2016 14:44 UTC
  • Kivuli cha mauti chawafunika maelfu ya watoto Afrika

Maelfu ya watoto wa maeneo tofauti ya Afrika wamefunikwa na kivuli cha mauti kutokana na ukosefu wa amani na machafuko yanayotokana na mashambulizi ya kigaidi na baa la njaa barani humo.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema kuwa, karibu nusu milioni ya watoto wa maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria wamo kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa iliyosababishwa na vita kati ya jeshi la serikali na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Mkurugenzi Mtendani wa UNICEF amesema, mgogoro wa njaa nchini Nigeria unaweza baadaye kubadilika kuwa janga la kibinadamu na kusisitiza kuwa, karibu watoto nusu milioni wa nchi hiyo wako katika hatari ya kupoteza maisha kwa njaa na jambo hilo ni sehemu ndogo tu ya hatari zinazowakabili wakimbizi milioni mbili na laki sita wa nchi hiyo.

Uongozi mbaya na vita ni miongoni mwa matatizo makubwa barani Afrika

 

Anthony Lake amesema, maafisa wa misaada ya kibinadamu hawana uwezo wa kuyafikia maeneo mengi ya jimbo la Borno, la kaskazini mashariki mwa Nigeria na kama hali hiyo itaendelea na watoto hao kuachwa wakiteseka kwa matatizo mbalimbali, basi kuna hatari khumusi nzima ya watoto hao wakapoteza maisha karibuni hivi. Mashirika ya misaada yanasema kuwa, watu milioni 4.4 wa maeneo hayo wanahitajia misaada ya haraka ya chakula na watu 65 elfu kati yao wanaishi katika mazingira ya ukame mkubwa.

Takwimu hizo zimetolewa katika hali ambayo hatari inayowakabili watoto ni ya kiwango hicho hicho kwenye nchi nyingine inayopakana na Nigeria yaani Niger. Wakimbizi wengi wanaokimbia mashambulizi ya Boko Haram huko Niger wako katika janga la njaa. 

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la magharibi mwa Afrika hivi karibuni alitahadharisha kuwa, makumi ya maelfu ya watu wanaishi kwenye eneo hilo ambalo wanamgambo wa Boko Haram wanafanya mashambulizi ya mara kwa mara, wanakabiliwa na kifo kutokana na ukame na njaa.

Waasi ni tatizo jingine kubwa barani Afrika

 

Hivi sasa miongo mitatu ya kilimo imepita bila ya wananchi wa eneo hilo kuweza kulima na kupanda mazao yoyote kutokana na kuhofia mashambulizi ya Boko Haram na wengi wao wamelazimika kuyakimbia maeneo yao.

Ripoti zinasema kuwa, zaidi ya watu laki tano ya 68 elfu wanakabiliwa na lishe duni katika pembe zote zinazopakana na Ziwa Chad na kuna hatari ya kupoteza maisha miezi michache ijayo kama hawatapelekewa chakula na madawa.

Tathmini ya usalama wa chakula iliyofanywa kwa mujibu wa vielelezo vya kimataifa inaonesha kuwa, sehemu kubwa ya wakazi wa eneo hilo wanaishi katika ukosefu mkubwa wa chakula na hivi sasa wako katika daraja ya tano ambayo kwa mujibu wa vielelezo hivyo hata wakipatiwa misaada ya kibinadamu bado wataendelea kukabiliwa na njaa, kifo na ukata wa kupindukia.

Mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram yaliyoanza miaka saba iliyopita yamepelekea zaidi ya watu 15 elfu kuuawa na milioni mbili wengine kuwa wakimbizi na licha ya nchi zinazopakana na Ziwa Chad kuunda kikosi cha pamoja na kupambana na kundi hilo, lakini hadi leo linaendeleza mashambuliai yake ya kikatili kwenye nchi kadhaa za eneo hilo.

Mashambulizi ya Boko Haram ni makubwa kiasi kwamba ni muhali kufikisha misaada kwa wakazi wa baadhi ya maeneo ya nchi hizo. Ukitoa Nigeria na Niger, maeneo mengine ya nchi zinazopakana na nchi hizo mbili nayo yana hali mbaya ya njaa, ukame na usalama mdogo.

Wakimbizi Ziwa Chad

 

Ukitoa upande wa magharibi mwa Afrika ambako genge la kigaidi la Boko Haram limesababisha maafa mengi, katika upande wa mashariki mwa Afrika pia hali ni ya hatari katika baadhi ya maeneo kutokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la al Shabab la nchini Somalia.

Kwa kuzingatia yote hayo tunaweza kusema kuwa, roho za mamia ya maelfu ya watoto wa maeneo mbalimbali ya Afrika zimegubikwa na kivuli hatari cha mauti na kama jitihada za kweli za kurejesha amani na hatimaye kutoa mwanya wa watu kuishi kwa salama na kujiendeshea maisha yao hazitachukuliwa, basi mgogoro unaowakabili watoto hao utageuka na kuwa janga kubwa la kibinadamu.