Juhudi zaidi za kuleta amani Sudan Kusini zinahitajika
-
Wanawake na watoto wadogo, wahanga wakuu wa machafuko ya Sudan Kusini
Mkuu wa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Makubaliano ya Amani ya Sudan Kusini ametaka juhudi zaidi zifanyike kwa ajili ya kurejea amani na utulivu nchini humo.
Festus Mogae, raia wa Botswana ametoa mwito huo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini na kuwataka viongozi wa nchi hiyo kuongeza juhudi za kuleta amani na utulivu nchini humo.
Mkuu huyo wa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Makubaliano ya Amani ya Sudan Kusini amesisitiza kwamba, kuna ulazima wa kuweko mavumiliano baina ya wananchi wa nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita na kuelezea matumaini yake kuwa pande hasimu za Sudan Kusini zitajali maslahi ya taifa na kufungua mlango wa mazungumzo zaidi ya maelewano.
Maelfu ya watu wameuawa, zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi na watu wengine milioni 4 na laki sita wanahitajia msaada wa haraka wa chakula kutokana na vita vya miaka mitatu vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.
Vita na machafuko yalipamba moto nchini humo baada ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kumtuhumu makamu wake Riek Machar kuwa anataka kumpindua mwaka 2013 na kuanzia hapa kukashuhudiwa maafa makubwa kwa wananchi wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Makubaliano ya mwisho ya amani ya Sudan Kusini yalifikiwa mwezi Agosti 2015 kati ya wafuasi wa Salva Kir na Riek Machar lakini hakuna upande wowote unaoheshimu makubaliano hayo.