Mgogoro wa kisiasa Kongo DR wapatiwa ufumbuzi?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21994-mgogoro_wa_kisiasa_kongo_dr_wapatiwa_ufumbuzi
Katika hatua ya ghafla na ambayo haikutazamiwa na wengi, pande hasimu za kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimefikia muafaka, ambao utapelekea Rais Joseph Kabila asalie uongozini hadi mwishoni mwa mwaka ujao 2017.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 23, 2016 16:24 UTC
  • Mgogoro wa kisiasa Kongo DR wapatiwa ufumbuzi?

Katika hatua ya ghafla na ambayo haikutazamiwa na wengi, pande hasimu za kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimefikia muafaka, ambao utapelekea Rais Joseph Kabila asalie uongozini hadi mwishoni mwa mwaka ujao 2017.

Martin Fayulu, mmoja wa viongozi wa upinzani Kongo DR ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, kwa mujibu wa makubaliano hayo, Rais Kabila ambaye muhula wake wa uongozi ulimalizika Disemba 20, atasalia mamlakani hadi mwishoni mwa mwaka ujao wa 2017, ambapo uchaguzi mkuu utaandaliwa. 

Rais Joseph Kabila wa Kongo DR

Aidha imeafikiwa kuwa mrengo wa upinzani utamteua Waziri Mkuu mpya, mchakato ambao utasimamiwa kwa karibu na kinara wa muungano mkuu upinzani nchini humo Mzee Etienne Tshisekedi ambaye atasimamia utekelezwaji wa makubaliano hayo.

Kadhalika makubaliano hayo yamebainisha kuwa, katiba ya nchi haitofanyiwa marekebisho kama ilivyokuwa imependekezwa awali na chama tawala na kwamba Rais Joseph Kabila hatoruhusiwa kugombea tena kiti cha rais baada ya kuongoza kwa mwaka mmoja.

Hata hivyo, Jean Marc Kabund, Katibu Mkuu wa chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini humo UDPS, ametahadharisha kuwa, makubaliano hayo hayajapata baraka kamili toka pande zote za kisiasa na wananchi. Aidha wawakilishi wa serikali katika mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Kanisa Katoliki, wamekataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu muafaka huo.

Mzee Etienn Tshisekedi, kinara wa upinzani DRC

Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umesema kuwa, zaidi ya watu 40 wameuawa katika ghasia na maandamano ya wananchi ya kushinikiza Rais Kabila aachie ngazi. Hayo yamesemwa na Zeid Ra'ad al-Hussein, Kaimishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ambaye ameongeza kuwa, watu 460 wamekamatwa na maafisa usalama kwa kushiriki maandamano hayo, yaliyopigwa marufuku na serikali ya Kinshasa.

Kwa mujibu wa katiba ya Kongo DR, Rais Joseph Kabila hastahiki kugombea kiti cha rais kwa mara nyingine baada ya kumalizika muhula wake wa uongozi mwezi huu wa Disemba. 

Maafisa wa polisi ya kupambana na ghasia Kinshasa