Burundi yapasisha sheria kali ya kuzidhibiti asasi za kigeni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22093-burundi_yapasisha_sheria_kali_ya_kuzidhibiti_asasi_za_kigeni
Bunge la Burundi limepasisha muswada wa sheria inayotaka kudhibitiwa asasi zisizo za kiserikali za kigeni, siku chache baada ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kudai kuwa asasi hizo zinafanya kampeni kubwa dhidi ya serikali yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 25, 2016 04:14 UTC
  • Burundi yapasisha sheria kali ya kuzidhibiti asasi za kigeni

Bunge la Burundi limepasisha muswada wa sheria inayotaka kudhibitiwa asasi zisizo za kiserikali za kigeni, siku chache baada ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kudai kuwa asasi hizo zinafanya kampeni kubwa dhidi ya serikali yake.

Spika wa Bunge hilo Pascal Nyabenda amesema muswada huo umepasishwa kwa kura 105 za ndio na moja ya hapana. Iwapo Rais Nkurunziza atapasisha muswada huo na kuwa sheria, asasi hizo ajinabi zitatakiwa kuweka pesa zao za kigeni katika akaunti zitakazolazimika kufungua kwenye Benki Kuu ambapo mzunguko wa fedha hizo utakuwa unatathminiwa kwa karibu na vyombo vya dola.

Aidha asasi hizo za kimataifa zitakiwa kulipa kiasi fulani kama pesa za kusajiliwa sambamba na kutakiwa kuandaa ripoti baada ya kila miezi sita kueleza namna zilivyotumia bajeti zao la sivyo ziwekewe vikwazo.

Umoja wa Ulaya, mmoja wa wafadhili wakuu wa Burundi

Wadadisi wa masuala ya uchumi wanasema kuwa, uamuzi huo huenda ukayumbisha uchumi wa nchi hiyo, haswa kwa kuzingatia kuwa baadhi ya wafadhili wakuu wa nchi hiyo maskini ya Afrika kama vile Umoja wa Ulaya wametishia kusitisha shughuli zao katika nchi hiyo, iwapo serikali haitasitisha machafuko, ukandamizaji dhidi ya wapinzani na wakosoaji wake na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa.

Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu mwaka jana 2015, kufuatia hatua ya Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu. Wapinzani kwa upande wao waliitaja  hatua hiyo ya Nkurunziza kuwa ni kinyume na katiba na kumtuhumu kuwa amepuuza makubaliano ya amani ya Burundi yaliyohitimisha vita vya ndani nchini humo.