Watatu wauawa, 26 wajeruhiwa katika mapigano ndani ya jela nchini Afrika Kusini
Watu watatu wameuawa na wengine 26 wamejeruhiwa katika mapigano yaliyotokea kati ya wafungwa na walinzi wa jela ya St. Albans katika bandari ya Elizabeth mkoani Cape ya Mashariki nchini Afrika Kusini.
Logan Maistry, msemaji wa Idara ya Huduma za Urekebishaji Mienendo amesema, yalitokea mapigano hapo jana baina ya wafungwa na walinzi wa jela na kusababisha watu watatu kuuawa na wengine 26 kujeruhiwa. Hata hivyo ameongeza kuwa haijafahamika mara moja ni wangapi wafungwa na wangapi ni walinzi wa jela waliouawa na kujeruhiwa katika machafuko hayo.
Polisi na timu za utoaji huduma za dharura walifika eneo la tukio huku ripoti zikieleza kuwa hali za majeruhi 10 ni mbaya.
Maafisa wa serikali wametangaza kuwa uchunguzi umeanzishwa kujua chanzo cha mapigano hayo na kwamba maafisa waandamizi akiwemo Waziri wa Sheria Michael Masutha wanatazamiwa kuitembelea jela hiyo hii leo.
Jela ya St Albans ina historia ya kushuhudia uasi na machafuko ya umwagaji damu ikiwemo uasi mkubwa wa mwaka 2013 wakati wafungwa walipowashambulia walinzi wa jela hiyo.
Wakati huohuo chama kikuu cha upinzani cha Muungano wa Kidemokrasia kimetoa wito wa kufanyika uchunguzi kamili huku kikiilaumu serikali kwa kuruhusu machafuko na uasi kutokea kwenye jela hiyo.
"Hii si mara ya kwanza kwa matukio ya utumiaji nguvu kutokea katika jela hii; hatuwezi kuruhusu matukio kama haya yaendelee kutokea bila ya kuwepo uwajibishaji", imeeleza taarifa iliyotolewa na chama hicho hapo jana…/