Dec 28, 2016 02:51 UTC
  • Polisi ya Uganda yafanya msako katika msikiti wa Nakasero

Kikosi cha Kupambana na Ugaidi cha Jeshi la Polisi nchini Uganda (JATT) jana Jumanne asubuhi kilifanya msako mkali katika msikiti wa Nakasero ulioko katika barabara ya Snay bin Amin jijini Kampala na kukamata watu kadhaa wakiwemo walinzi wa msikiti huo.

Mashuhuda wanasema maafisa usalama hao waliuvamia msikiti huo na kuuzingira kwa masaa kabla ya kuondoka na matarakilishi na vyeti vilivyotajwa na uongozi wa msikiti huo kuwa nyeti.

Habib Buwembo, mmoja wa wasemaji wa msikiti huo amesema maafisa hao walivunja milango ya ofisi ya msikiti huo na kuchukua kompyuta, stakabadhi muhimu, pikipiki sita na shilingi milioni 50 zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Jumba la Ummah

Waislamu Uganda

Kadhalika amebainisha kuwa walinzi 11 wa msikiti huo walikamatwa wakati wa msako huo na hadi tunaenda mitamboni familia zao zilikuwa zinasema hazijui waliko.

Msemaji wa Polisi Andrew Felix Kaweesi amethibitisha kufanyika kwa msako huo na kueleza kuwa maelezo ya kina yatatolewa katika siku zijazo. Haijafahamika ikiwa msako huo, unahusishwa na kukamatwa kwa viongozi wakuu wa harakati ya Jamat Dawatil Salafiya au la.

Kumekuwa na hali ya wasiwasi katika msikiti huo baada ya kukamatwa kwa viongozi wa  Jamat Dawatil Salafiya akiwemo Sheikh Yahaya Mwanje na Katibu Mkuu Ayub Nyende miongoni mwa wengine. Viongozi hao walikamatwa wakihusishwa na mauaji ya Sheikh Major Muhammad Kiggundu Novemba 26, mbali na viongozi wengine wengi wa Kiislamu nchini humo.

Tags