Wanajeshi 2 wa Misri wauawa katika shambulizi la bomu Sinai
Kwa akali askari 2 wa Misri wameuawa katika shambulio la bomu katika Peninsula ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika.
Aidha askari mmoja amejeruhiwa katika shambulizi hilo la bomu lililolenga gari la jeshi katika mji wa al-Arish, kaskazini mwa eneo la Sinai. Hakuna kundi lolote la kigaidi limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya bomu ya jana Jumamosi.
Wiki mbili zilizopita, magaidi wanaofungamana na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh nchini Misri waliua raia 16 huko Sinai kwa tuhuma za kushirikiana na jeshi la serikali. Kabla ya hapo, askari 8 waliuawa katika shambulio la bomu huko Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Kundi hilo ambalo zamani likijulikana kama Ansar Bait al Maqdis ambalo mwaka 2014 lilitangaza utiifu kwa kundi la kigaidi la ISIS ndilo limekuwa likitekeleza hujuma za namna hii dhidi ya raia na maafisa usalama katika eneo hilo.
Kwa mara kadhaa kundi hilo limekuwa likitekeleza hujuma dhidi ya askari wa usalama wanaoendesha operesheni za kulisafisha eneo la Sinai tangu alipoondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Muhammad Mursi hapo mwezi Julai mwaka 2013.
Hali ya hatari ilitangazwa katika eneo hilo la Sinai mwaka 2014, baada ya wanajeshi 30 kuuawa katika shambulizi jingine la kigaidi.