Chama kikuu cha upinzani Msumbiji charefusha muda wa usitishwaji vita
Chama kikuu cha upinzani nchini Msumbiji kimetangaza kurefusha muda wa usitishaji vita kati yake na serikali kwa muda wa miezi miwili, ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya amani.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Renamo ambaye yuko mafichoni, Afonso Dhlakama amesema leo Jumanne kuwa, wameamua kuchukua uamuzi huo ili kupunguza mauaji ya raia sambamba na kuvalia njuga mazungumzo kati ya wapinzani na serikali ya Rais Filipe Nyusi wa nchi hiyo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, chama cha upinzani cha Renamo kilitangaza kuwa, kitasitisha operesheni zake za kijeshi dhidi ya vikosi vya serikali kwa muda wa siku saba ili kuheshimu sherehe za mwaka mpya.
Kiongozi wa chama hicho cha Renamo ambacho kwa miaka kadhaa sasa kimekuwa kikiendesha mapigano dhidi ya serikali aliwaambia waandishi wa habari kwamba, ili kutoa fursa kwa wananchi wa Msumbiji kuadhimisha sherehe za mwaka mpya, chama chake kingesitisha operesheni zake za kijeshi dhidi ya vikosi vya serikali kwa muda wa siku saba.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanakadiria kwamba, makumi ya watu waliuawa mwaka wa 2016 kufuatia mapigano kati ya wapiganaji wa chama cha Renamo na chama tawala nchini Msumbiji cha Frelimo.
Inaarifiwa kuwa, watu zaidi ya milioni moja waliuawa katika mapigano baina ya pande mbili hizo hasimu kati ya mwaka 1976 na 1992.