Rais wa Sudan Kusini: Askari wanaobaka inapasa wauawe
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema askari wanaowabaka raia inapasa wauawe kwa kupigwa risasi. Rais Kiir alitangaza msimamo huo jana katika hotuba aliyotoa wakati alipotembelea mji wa Yei.
"Wale wanaofanya vitendo vilivyo kinyume na sheria, wanaobaka wanawake na wasichana, hii si sera ya serikali …. mwili wa mwanamke hauwezi kuchukuliwa kwa nguvu", amesema Rais wa Sudan Kusini, kauli ambayo inaonekana ni ya kujaribu kuwapoza raia waliokasirishwa na vitendo viovu vinavyofanywa na vikosi vya usalama na vile vile kuzima hasira zinazoongezeka kimataifa dhidi ya hujuma hizo wanazofanyiwa raia hao.
"Kuanzia sasa na kuendelea, ninamtaka Mkuu wa Majeshi Jenerali Paul Malong na Waziri wa Ulinzi waripoti kwangu endapo kitendo kama hiki kitatokea. Katika kesi kama hii tutampiga risasi aliyefanya hivyo", amesisitiza Rais Kiir.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema, askari wa jeshi la serikali wamekuwa wakishirikiana kimakundi kubaka wanawake kwa msingi wa kikabila. Kesi chache za ubakaji zimeripotiwa kuwakuhusisha pia wanamgambo wa mrengo wa waasi.
Ripoti za ukatili wa kingono unaofanywa bila wahusika kufuatiliwa kisheria zimezusha mvutano kati ya serikali ya Sudan Kusini na wafadhili wa Magharibi wanaochangia karibu mahitaji yote ya sekta za afya na elimu ya nchi hiyo pamoja na kugharamia kikosi cha askari 15,000 walinda amani wa Umoja wa Mataifa kinachotumia karibu dola bilioni moja kwa mwaka…/