SADC: Burundi imalize mgogoro wa kisiasa ili ipewe uanachama
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25736-sadc_burundi_imalize_mgogoro_wa_kisiasa_ili_ipewe_uanachama
Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC imeitaka Burundi kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoikabili kwa sasa, iwapo inataka kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 28, 2017 03:51 UTC
  • SADC: Burundi imalize mgogoro wa kisiasa ili ipewe uanachama

Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC imeitaka Burundi kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoikabili kwa sasa, iwapo inataka kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Tanzania, Augustine Mahiga amesema ombi la Burundi la kutaka kupewa uanachama wa SADC lilijadiliwa katika mkutano wa Februari 24 mjini Dar es Salaam, ambapo Kamati ya Ushirikiano wa Siasa, Diplomasia, Ulinzi na Usalama ya jumuiya hiyo  ilipendekeza kuwa, kadhia hiyo ijadiliwe baadaye mambo yakishatangamaa nchini Burundi.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Burundi ilisusia mazungumzo ya kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo yaliyofanyika Februari 16 mjini Arusha, Tanzania.

Dakta Mahiga

Phillipe Nzobonariba, Msemaji wa Serikali ya Burundi alisema kuwa, pamoja na masuala mengine, upande wa serikali ulimua kutoshiriki mazungumzo hayo kulalamikia uwepo wa mshauri wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, Benomar Jamal katika mazungumzo hayo, na kwamba mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Benjamin Mkapa, Rais wa zamani wa Tanzania, yatatatiza juhudi za kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.

Machafuko na umwagaji damu ulianza kushuhudiwa nchini Burundi mwezi Aprili mwaka 2015 na kushtadi baada ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuamua kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo, hatua ambayo wapinzani wanasema ni kinyume na katiba na makubaliano ya amani yaliyofikiwa mjini Arusha, Tanzania.

Rais Nkurunziza wa Burundi

Wadasisi wa mambo wanasema kuwa, iwapo Burundi itajiunga na Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, hatua hiyo itavuruga muelekeo na ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.