Askari 10 wa Misri wauawa katika hujuma ya bomu Sinai
Wanajeshi zaidi ya 10 wa Misri wameuawa baada ya gari walimokuwa kulengwa kwa shambulio la bomu katikati mwa Peninsula ya Sinai.
Msemaji wa jeshi la Misri amesema kuwa, wanajeshi hao waliuawa katika operesheni ya jana ya kuzisafisha ngome za magenge ya kigaidi eneo la Sinai.
Amebainisha kuwa, vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika vimefanikiwa kuwaangamiza magaidi 15 katika operesheni hiyo, mbali ya kuwatia mbaroni wengine 7.
Kadhalika msemaji huyo wa jeshi la Misri amesema kuwa, maafisa usalama wa nchi hiyo wamefanikiwa kuharibu mada za miripuko ikiwemo nusu tani ya TNT, sambamba na kunasa maguruneti, mamia ya simu za rununu na magari mawili yaliyokuwa yakitumiwa na magaidi hao.
Kanali ya televisheni ya Sky News hapo jana iliripoti kuwa, magaidi wasiopungua watano wameuliwa na wanajeshi wa Misri katika eneo la Jabal al Hilal, kusini mwa mji wa al Arish, katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
Eneo la Sinai Kaskazini limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi la Ansar Baytul Muqaddas, tawi la genge la kigaidi la Daesh nchini Misri.