Mar 31, 2017 14:55 UTC
  • Machafuko yashtadi Kongo DR, Angola yafunga mpaka wake na nchi hiyo

Serikali ya Angola imeamua kufunga mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na kushtadi machafuko katika mkoa wa Kasai, kusini mwa DRC.

Ernesto Muangala, Gavana wa mkoa wa Lunda Norte ulioko umbali wa kilomita 656 kaskazini mwa mji mkuu, Luanda na wenye mpaka wa pamoja na Kongo DR na Kongo Brazaville amesema kuwa, kutokana na kuongezeka machafuko katika mkoa wa Kasai, mpakani mwa nchi hiyo na DRC, wamelazimika kufunga masoko na shughuli zote katika eneo hilo.

Mkoa wa Kasai umekuwa ukishuhudia machafuko tangu Septemba mwaka jana, ambapo watu zaidi ya 400 wameuawa katika machafuko na mapigano kati ya askari usalama na wanamgambo wanaomuunga mkono kiongozi wao wa zamani Kamuina Nsapu, aliyeua na maafisa usalama.

Waasi wapiganaji wa msituni Kongo DR

Ni katika mkoa huohuo wa Kasai, ambako miili ya maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa raia wa Marekani na Sweden waliotekwa nyara na waasi wiki mbili zilizopita ilipatikana Jumanne wiki hii. Kabla ya hapo, maafisa polisi 40 wa Kongo DR waliuawa kwa kukatwa vichwa katika eneo hilo.

Hii ni katika hali ambayo, upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umewataka wananchi wa nchi hiyo kuketi majumbani mwao Jumatatu ijayo na kutotoka nje ili kumlazimisha Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kutekeleza makubaliano ya kugawana madaraka. Umesema machafuko ya sasa nchini humo yamesababishwa na hatua ya Rais Kabila ya kukataa kutekeleza makubaliano ya kugawana madaraka yaliyotiwa saini Disemba 31 mwaka jana. 

 

Tags