Apr 09, 2017 14:22 UTC
  • Watu 15 wauawa katika mlipuko wa bomu Mogadishu, Somalia

Watu wasiopungua 15 wameuawa baada ya bomu lililotegwa ndani ya gari kuripuka nje ya kambi ya jeshi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Duru za polisi zinasema kuwa, bomu hilo limeripuka nje ya jengo lenye ofisi za Wizara ya Ulinzi ambapo mbali na maafa hayo, watu wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Habazi zaidi zinasema kuwa, hujuma hiyo ililenga msafara wa Mkuu mpya wa Majeshi, Jenerali Mohamed Ahmed Jimale pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa usalama.

Meja Hussein Nur, kamanda wa jeshi la Somalia amethibitisha kutokea shambulizi hilo la kigaidi, ambalo limeua abiria wote waliokuwa katika basi moja dogo, pamoja na maafisa usalama kadhaa.

Sehemu ya athari za hujuma za al-Shabaab Somalia

Usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita, watu zaidi ya 20 waliuawa baada ya bomu lililotegwa kando ya barabara kuripuka wakati basi dogo la abiria lilipokuwa likipita katika eneo la Shebelle ya Chini katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Mashambulizi haya ya kigaidi yanayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni, Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo alitangaza kuwa nchi hiyo ni eneo la vita, huku akitoa siku 60 kwa wanamgambo wa al-Shabaab waweke silaha chini na wajisalimishe.

Tags