Wakristo waungana na Waislamu Nigeria kushinikiza kuachiwa huru Zakzaky
Kwa mara nyingine tena Waislamu nchini Nigeria wamefanya maandamano ya amani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja kushinikiza kuachiwa huru mwanazuoni wa Kiislamu nchini humo, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Hata hivyo maandamano hayo yaliyofanyika jana yalikuwa ya aina yake, kwa kuwa yalipata uungaji mkono kutoka kwa waandamanaji Wakristo.
Mwandishi wa habari wa kanali ya televisheni ya Press TV ameripoti kuwa, waandamanaji hao bila kujali tofauti zao za kidini chini ya mwavuli wa Concerned Nigerians, wamesema zimepita takriban siku 485 tangu kukamatwa na kuzuiliwa kwa kiongozi na mwanaharakati huyo wa kidini, mkewe na wafuasi wake wengine kinyume cha sheria na siku 130 tangu Mahakama ya Federali ya nchi hiyo iagize kuachiwa kwao huru.
Hata hivyo maandamano hayo yalitibuka baada ya polisi ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kuwarushia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji hao sambamba na kuwamwagia maji.
Wiki iliyopita, wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria wakiwa pamoja na wanafunzi na wanachuo wa taasisi mbali mbali za elimu nchini humo, waliandamana kwa amani na kisha kupiga kambi nje ya manjengo ya Bunge katika mji mkuu Abuja, ambapo wamekabidhi waraka wa matakwa yao kwa afisa mmoja wa Bunge.
Licha ya muhula uliotolewa na Mahakama ya Federali kwa ajili ya kuachiliwa huru msomi na mwanaharakati huyo wa kidini kumalizika tarehe 16 Januari mwaka huu, lakini serikali haijatekeleza amri hiyo. Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa tarehe Pili Disemba mwaka jana na mahakama hiyo, kitendo cha kuendelea kushikiliwa na serikali ya nchi hiyo Sheikh Zakzaky, mke na wanaharakati wengine wa Kishia ni kinyume cha sheria.