Chama tawala Kenya chafutilia mbali zoezi la mchujo baada ya kuibuka vurugu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28094-chama_tawala_kenya_chafutilia_mbali_zoezi_la_mchujo_baada_ya_kuibuka_vurugu
Chama tawala cha Jubilee nchini Kenya kimefutilia mbali zoezi la uteuzi wa nafasi za wagombea wake katika Kaunti zote baada ya kushuhudiwa vurugu na machafuko hapo jana.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Apr 21, 2017 23:40 UTC
  • Chama tawala Kenya chafutilia mbali zoezi la mchujo baada ya kuibuka vurugu

Chama tawala cha Jubilee nchini Kenya kimefutilia mbali zoezi la uteuzi wa nafasi za wagombea wake katika Kaunti zote baada ya kushuhudiwa vurugu na machafuko hapo jana.

Katibu mkuu wa chama hicho Bwana Raphael Tuju amesema kuwa, chama hicho leo kinatarajiwa kutangaza tarehe mpya za uchaguzi huo. Bwana Tuju hapo awali alikuwa amesema kuwa baada ya mazungumzo na viongozi wakuu wa chama hicho , ilikubaliwa kwamba uchaguzi huo uahirishwe hadi siku nyengine ili kuweka uwazi na usawa.

Uteuzi wa wagombea ulikuwa umesitishwa katika kaunti za Narok, Kajiado, Kericho, Bomet, Uasin Gishu,Trans Nzoia ,Baringo, Nakuru, Elgeyo marakwet, Nandi, Embu, Kiambu, Murang'a, Kirinyaga na Nyeri

Wafuasi wenye hasira wa Jubilee wakichoma moto karatasi za kupigia kura

Uchaguzi huo ulikabiliwa na visa vya uchomaji wa vifaa vya kupigia kura, mgomo wa wapiga kura huku kukiwa na hofu ya wizi wa kura na vitisho vya kuhamia vyama vyengine. wafuasi wengi wa chama hicho walikuwa wakilalamikia uchache wa karatasi za kupigia kura na vile vile kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura. Katika baadhi ya maeneo vurugu zilikuwa kubwa ambapo vijana wenye hasira waliweka vizuizi barabarani huku wengine wakivamia vituo vya kupigia kura na kuchoma moto makaratasi ya kupigia kura.

Wiki iliopita shughuli kama hiyo ilifanyika katika chama cha upinzani cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ambapo kulikuwa na ghasia katika maeneo ya magharibi mwa Kenya.