Mar 11, 2016 01:43 UTC
  • Ban ataka askari waliobaka wanawake waadhibiwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya askari wa kulinda amani wa kimataifa waliohusishwa na vitendo vya kunajisi wanawake.

Ban Ki-moon ambaye jana alikuwa akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York alisema kuwa, askari walionajisi na kubaka wanawake wanapaswa kupandishwa kizimbani na kuhukumiwa.

Wito huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa umetolewa baada ya kukithiri vitendo viovu kama hivyo vya askari wa kimataifa wa kilinda amani katika nchi mbalimbali hususan huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Baadhi ya nchi pia zinatuhumiwa kuwa hazichukui hatua za kutosha dhidi ya askari wao waliohusishwa na vitendo viovu vya kunajisi au kutumia vibaya wanawake wakiwa katika majukumu yao ya kulinda amani.

Nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Mataifa zimependekeza muswada katika Baraza la Usalama la umoja huo zikitaka kurudishwa nyumbani askari wote wanaotuhumiwa kubaka wanawake au kuhusika na ukatili wa kingono.

Tags