Iran na Tanzania kuimarisha uhusiano wao katika uwekezaji wa nishati
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Tanzania zimekusudia kuimarisha uhusiano baina yao katika sekta ya uwekezaji wa nishati.
Hayo yameelezwa katika mazungumzo baina ya balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania, Mousa Farhang na Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, baada ya balozi huyo kumtembelea waziri huyo ofisini kwake mjini Dodoma.
Katika ziara hiyo ambayo pia ilikuwa na lengo la kujitambulisha, viongozi hao walizungumzia suala la kuimarishwa uhusiano ya nchi mbili hususan katika sekta za nishati na madini.
Akizungumzia azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kushirikiana na nchi za Kiafrika ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya nishati, balozi Farhang amemwambia Waziri Muhongo kuwa, Tehran ina uwezo mkubwa katika sekta hiyo na kuongeza kuwa, mbali na kuzalisha umeme wa kutosha kwa mahitaji ya nchi, imeweza pia kujenga viwanda mbalimbali vya umeme katika baadhi ya nchi zinazoizunguka Iran.
Kadhalika balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania, amemwambia Waziri Muhongo kwamba, Iran huzalisha zaidi ya mapipa milioni nne ya mafuta kwa siku. Amesema, Hivi sasa Iran tunazalisha umeme mwingi unaotosheleza mahitaji ya nchi yetu na mwingine tunauza nje." Balozi wa Iran nchini Tanzania ameongeza kuwa, kutokana na utafiti alioufanya yeye binafsi, amegundua kuwa, sekta ya nishati ndiyo yenye nafasi kubwa na nzuri zaidi itakayowezesha nchi za Iran na Tanzania kunufaika endapo zitashirikiana.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo amemuhakikishia balozi wa Iran kwamba, serikali ya nchi hiyo iko tayari kupokea uzoefu wa Tehran katika uga huo. Kadhalika waziri Muhongo ameonyesha kufurahishwa sana na ziara hiyo ya balozi Farhang na kuongeza kuwa, ni muda mrefu sasa Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na Iran.