Ajali mbaya yaua wanafunzi 32 na walimu wao mjini Arusha Tanzania
Polisi ya Tanzania imetangaza kutokea ajali mbaya iliyosababisha jumla ya wanafunzi 29, walimu wawili na dereva mmoja kufariki dunia.
Taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoani Arusha, Kaskazini mwa Tanzania imesema kuwa, jumla ya wanafunzi 32 pamoja na walimu wao wamepoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea wilani Karatu kando ya Mto Marera.
Kamanda wa polisi mkoani humo, Charles Mkumbo amesema kuwa, wanafunzi hao ni wa shule ya Lack Vicent ya mkoni hapo na walikuwa wanenda kushiriki mtihani na wanafunzi wenzao wa shule ya Tumaini English Medium ya mjini Karatu. Habari za awali zimesema kuwa ni watoto wanne pekee ndio walionusurika katika ajali hiyo ingawa hali zao ni mahututi na kwamba kuna uwezekano idadi ya vifo ikaongezeka.
Ajali hiyo imetokea baada ya basi aina ya Coaster walilokuwa wakisafiria, kuacha njia na kutumbukia mtoni, katika mlima Rhotia, kwenye Mto Marera. Wakati huo huo, habari za hivi punde kutoka hospitali ya Lutheran mjini Karatu zinasema kuwa miili 32 ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo imepokelewa katika hospitali hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, miili miwili ni ya walimu wawili, dereva mmoja na wanafunzi 29, ambapo 11 ni wavulana na wasichana 18.
Kufuatia tukio hilo, Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo na kueleza kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa na imesababisha uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na taifa kwa ujumla.