May 10, 2017 14:21 UTC
  • Rais wa Niger: Zichukuliwe hatua za kukabiliana na ukosefu wa usalama Afrika

Rais Mahamadou Issoufou wa Niger ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti kwa ajili ya kukabiliana na ukosefu wa usalama na wakati huo huo kuungwa mkono suala la haki za binadamu barani Afrika.

Rais Mahamadou Issoufou  amesema hayo katika hotuba yake kwenye Kikao cha Sitini cha Kamisheni ya Haki za Binadamu na Watu ya Umoja wa Afrika (ACHPR) kinachofanyika katika mji mkuu wa Niger, Niamey kwa kuhudhuriwa na wawakilishi zaidi ya 600 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na za mabara mengine duniani.

Rais wa Niger ameeleza kusikitishwa kwake na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na makundi mbalimbali hususan magenge ya wahalifu, makundi ya kigaidi na makundi mbalimbali ya wanamgambo barani Afrika. Rais Mahamadou Issoufou  amesema kuwa,  kutopewa umuhimu wowote maisha ya watu na haki za binadamu kuanzia Libya mpaka Mali, kutoka Bonde la Ziwa Chad hadi Somalia na kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini mpaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni mambo yanayosikitisha mno.

Wanachama wa moja ya makundi ya waasi yanayohatarisha usalama DRC

Aidha katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais wa Niger amesema kuwa, kuteketezwa roho za raia pamoja na vitendo vya ubakaji, ukatili na unyanyasaji wanavyofanyiwa raia hao vinatia wasiwasi.

Kikao cha Sitini cha Kamisheni ya Haki za Binadamu na Watu ya Umoja wa Afrika kinafanyika katika hali ambayo, idadi kubwa ya raia wa nchi mbalimbali za bara hilo wanaishi katika mazingira yasiyo na usalama na uthabiti na yaliyogubikwa na wingu la vita na mapigano, huku wengine wengi wakiwa wahanga na waathirika wa vitendo vya makundi ya kigaidi pamoja na hali mbaya za kisiasa zinazotawala katika nchi zao.

Tags