May 16, 2017 12:51 UTC
  • Kuendelea vurugu na mivutano nchini Ivory Coast

Sambamba na kuendelea mapigano na vitisho vya wanajeshi waasi katika miji kadhaa nchini Ivory Coast, shughuli za benki, shule na vituo vya biashara zimesitishwa katika miji kadhaa ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa zinasema kuwa, wanajeshi waasi wanadhibiti maeneo muhimu ya miji ya Yamoussoukro, San-Pédro, Bouaké na Abidjan katika hali ambayo, mkuu wa majeshi ya nchi hiyo alikuwa amewataka wanajeshi hao waweke silaha chini la sivyo wajiandae kukabiliwa na nguvu za jeshi. Wanajeshi hao wameanzisha uasi wakilalamikia kucheleweshwa kulipwa malimbikizo yao ya marupurupu. 

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi michache kushuhudiwa uasi wa wanajeshi nchini Ivory Coast. Malalamiko ya uasi ya wanajeshi hao ambao wengi wao katika mji wa Bouake walimsaidia Rais Ouattara kuingia madarakani yalianzia katika mji huo ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo na kuenea hadi Abidjan na miji mingine.

Wanajeshi waasi wa Ivory Coast

Mwezi Januari mwaka huu kulishuhudiwa uasi kama huo, hata hivyo ulifikia tamati baada ya mazungumzo ya maafisa wa ngazi za juu na wanajeshi hao waasi na ahadi za Rais Alassane Ouattara za kulipwa marupurupu wanajeshi hao, kupatiwa nyumba na kuongezewa mshahara. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, uasi wa mara hii wa wanajeshi ni wa kulalamikia kutotekelezwa ahadi zilizotolewa na Rais Alassane Ouattara.

Huku vuta nikuvute hiyo ikiendelea baina ya wanajeshi waasi na serikali, nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na hali mbaya ya uchumi unaolegalega huku raia wengi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika wakilalamikia hali hiyo. Kuporomoka bei ya kakao ambalo ndilo zao muhimu linaloipatia kipato nchi hiyo kutokana na kuuzwa nje ya nchi, kunatajwa na wajuzi wa mambo kuwa, kumepelekea kupungua bajeti ya nchi na matokeo yake ni kuchelewa kulipwa mishahara wanajeshi na wafanyakazi wa baadhi ya idara za serikali. 

Aidha kufanyiwa marekebisho sheria ya kustaafu kumeitwisha serikali mzigo mkubwa wa fedha huku mazingira yakiwa magumu mno kwa wafanyakazi wastaafu. Ivory Coasti inakumbwa na matatizo hayo katika hali ambayo, kuboreshwa hali ya uchumi, kuanzisha nafasi za ajira na kupunguza umasikini ndizo zilizokuwa ahadi kuu za Rais Alassane Ouattara katika kampeni zake za uchaguzi. Sio tu kwamba, matatizo hayo hayajapatiwa ufumbuzi, bali filihali nchi hiyo inakabiliwa na ukosefu wa uthabiti wa kisiasa.

Rais Alassane Ouattara

Hata kama kufanyika uchaguzi na kupatikana usalama wa sasa wa nchi hiyo kunahesabiwa kuwa ni hatua moja kubwa ya kisiasa nchini Ivory Coast, lakini wapinzani nchini humo wamaendelea na harakati zao katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka Rais Alassane Ouattara ajiuzulu na kuachia ngazi. 

Hivi sasa kutokana na nchi hiyo kuwahi kushuhudia mapinduzi ya kijeshi, kumezuka wasiwasi wa kukaririwa tena tukio kama hilo nchini humo. Licha ya kuwa wanajeshi waasi wametangaza wazi kwamba, wako pamoja na Rais Alassane Ouattara na wanachodai wao ni kuboreshwa tu hali yao, lakini mvutano wa sasa umeongeza wasiwasi wa kutokea mapinduzi katika nchi hiyo. 

Wanajeshi waasi Ivory Coast

Vitisho vya ugaidi na hatari ya uingiliaji wa madola ya kikoloni katika masuala ya ndani ya Ivory Cost nalo ni tishio jingine muhimu dhidi ya nchi hiyo. Ivory Coast ni moja ya nchi zinazotazamwa kwa jicho la tamaa na Ufaransa  na bila shaka aina yoyote ya mvutano wa ndani na ukosefu wa usalama unaweza kumpatia mkoloni huyo wa zamani kisingizio cha kuingia tena nchini humo.

Aidha uwepo wa makundi ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya bara la Afrika kumeongeza wasiwasi wa kupanuka harakati za makundi ya kigaidi katika nchi ambazo zinakabiliwa na machafuko na migogoro.

Kwa sasa jambo la msingi ni wawakilishi wa serikali kufikia makubaliano na wanajeshi hao waasi ili kuzuia nchi hiyo kutumbukia tena katika vita na machafuko ya ndani. 

Tags