May 17, 2017 13:49 UTC
  • Jeshi la DRC laangamiza ngome ya wanamgambo wa Mai-Mai

Mapigano makali yameripotiwa kutokea baina ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wanamgambo wa Mai-Mai katika mkoa wa Kivu Kusini ulioko mashariki mwa nchi hiyo ambapo jeshi limefanikiwa kuangamiza ngome moja ya waasi hao.

Duru za kijeshi zimetangaza kuwa, mapigano kati ya pande mbili yalijiri katika eneo la Kilogoza katika mkoa wa Kivu Kusini ambapo kwa akali wanachama wawili wa kundi la waasi wa Mai- Mai wameuawa huku bunduki mbili aina ya AK 47 zikinaswa katika tukio hilo.

Wakati huo huo habari nyingine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinasema kuwa, idadi ya wafungwa wasiojulikana wameuawa kwa kupigwa risasi katika nchi hiyo mapema leo katika jaribio la kutaka kutoroka kutoka katika gereza kubwa lililoko mjini Kinshasa.

Waziri wa sheria nchini humo, Alexis Thambwe Mwamba amesema kuwa, baadhi ya wafungwa wapatao 100 wamekamatwa huku wengine hamsini na watano wakiendelea kusakwa.

Gereza la Makala mjini Kinshasa

Miongoni mwa wanaodaiwa kufanikiwa kutoroka ni mfungwa mmoja aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha gerezani kwa mauaji ya rais wa zamani wa DRC, Laurent Kabila.

Maafisa wa usalama wameanzisha oparesheni kali mjini Kinshasa ili kuwakamata wafungwa hao. Aidha, baadhi ya wafungwa wameuawa kwa kupigwa risasi wakijaribu kukimbia. 

Hii sio mara ya kwanza kwa wafungwa kutoroka kutoka magereza nchini DRC kwani Januari mwaka uliopita, kisa kama hicho kilishuhudiwa mashariki mwa taifa hilo ambapo wafungwa hamsini walitoroka. 

Mamlaka za magereza zimelaumiwa kwa visa hivyo kwa ulegevu huku magereza mengi yakiwa na msongamano.

Tags