Askari polisi 5 wa Kenya wauawa katika shambulizi la bomu
Kwa akali maafisa watano wa polisi nchini Kenya wameuawa katika shambulizi la bomu lililotokea leo Alkhamisi eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Mohamud Ali Saleh, Mshirikishi wa eneo la Kaskazini Mashariki amesema maafisa hao wa polisi ya utawala wameuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu lililokuwa limetegwa ardhini katika eneo la Liboi, kaunti ya Garissa, katika mpaka wa nchi hiyo na Somalia.
Amesema shambulizi hilo ambalo genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limekiri kuhusika nalo limejiri katika barabara ya Malelei-Kulan katika eneo la Liboi, kaunti ya Garissa na kuongeza kuwa maafisa wawili wa polisi wamejeruhiwa vibaya katika hujuma hiyo.
Hujuma hii inajiri siku moja baada ya maafisa wengine wanane wa usalama kuuawa katika mashambulizi mawili ya bomu katika kaunti za Mandera na Garissa, katika eneo hilo la kaskazini mashariki, huku hujuma ya Mandera ikilenga msafara wa Gavana wa kaunti hiyo Ali Roba.
Wimbi hili la mashambulizi dhidi ya maafisa usalama nchini Kenya linajiri katika hali ambayo, hivi karibuni, Joseph Boinnet, Inspekta Jenerali wa Polisi nchini humo alitahadharisha kuwa baadhi ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wamepenyeza nchini kwa ajili ya kuvuruga usalama wa taifa, na kuwataka wananchi kuwa macho na kuripoti matukio yoyote wanayohisi yanaweza kuhatarisha usalama kwa vyombo husika.