Burundi yachukua hatua kudhibiti mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana
Serikali ya Burundi imewaagiza watu wote hususan vijana wanaoishi kinyumba kuhalalisha na kusajili ndoa zao kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Hatua hii ni muendelezo wa kampeni ya kudhibiti mmomonyoko wa maadili iliyoanzishwa na Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo miaka kadhaa iliyopita. Terence Ntahiraja, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Burundi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, taifa hilo linakabiliwa na kile alichokitaja kama 'mlipuko wa idadi ya watu' kutokana na vijana kujihusisha na mahusiano haramu, yaliyopelekea mamia ya mabinti kupata ujauzito wakiwa bado shuleni.
Amesema ndoa halali sio tu suluhu ya kudhibiti mmomonyoko wa maadili unaoshuhudiwa nchini humo bali pia ni jukumu la kizalendo. Kadhalika amesisitiza kuwa, kampeni hiyo inayoendeshwa na serikali inafuata sheria kikamilifu na wala haikiuki haki za binadamu.
Gavana wa Mkoa wa Rutana, kusini mashariki mwa Burundi amewataka watu wa jinsia mbili wanaoishi pamoja pasina na ndoa halali wafanye juu chini kuhalalisha ndoa zao kufikia Juni 22, vinginevyo watatozwa faini ya Franca 50,000 za Burundi sawa na Yuro 22.
Katika mkoa wa Ngozi, kaskazini mwa nchi, watoto wanaozaliwa nje ya ndoa hawapewi elimu na matibabu ya bure ili kuzuia vijana kujihusisha na ngono zembe.
Rais Nkurunziza alianzisha kampeni hii Agosti mwaka 2013, kwa lengo la kuimarisha 'thamani chanya za kiutamaduni'.